Nairobi Utd yatangulia CAF ikiwatoa Waganda
Muktasari:
- Wajanja hao wa Nairobi imelazimisha sare ya 1-1 dhidi ya NEC FC ya Uganda na kuwang'oa wapinzani wao hao kwa faida ya bao la ugenini baada ya wiki iliyopita kutoka sare ya 2-2 ugenini.
Bao la dakika ya 65 kupitia Duncan Omala limeiwezesha Nairobi United kutoka sare jioni hii ikiwa nyumbani na kuwa timu ya kwanza ya Kenya kufuzu raundi ya pili ya michuano ya CAF.
Wajanja hao wa Nairobi imelazimisha sare ya 1-1 dhidi ya NEC FC ya Uganda na kuwang'oa wapinzani wao hao kwa faida ya bao la ugenini baada ya wiki iliyopita kutoka sare ya 2-2 ugenini.
Wageni NEC ilitangulia mapema kipindi cha kwanza kwa bao la dakika ya 26 kupitia nyota wao aitwae Waibi na kudumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Nairobi Utd ilicharuka na kutengeneza nafasi kadhaa za mabao kupitia nyota wa timu hiyo kabla ya Omala kutumbukiza mpira wavuni dakika ya 65 akiisawazishia wenyeji.
Hadi 90 zikikamilika matokeo yalikuwa bao 1-1 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 baada ya sare ya 2-2 ya wikiendi iliyopita jijini Kampala na kuivusha Nairobi hadi raundi ya pili ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kesho Jumapili mabingwa wa Kenya, Polisi itakuwa kibaruani kurudiana na Mogadishu City ya Somalia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi iliyopita ikiwa ugenini vijana wa kocha Etienne Ndayiragije ilishinda kwa mabao 3-1 na kesho itahitaji sare yoyote kutinga raundi ya pili kuungana na ndugu zao wa Nairobi United waliotangulia sambamba na Kaizer Chiefs, Dekedda ya Somalia, KMKM, Ferreviario Maputo, Royal Leopards na Al Ittihad ya Libya.