Kampala yaichapa Denden 7-0 CECAFA
Muktasari:
- Mechi ya kwanza Kampala ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya wenyeji wa mashindano hayo, Police Kenya ambayo ina mechi moja mkononi.
KAMPALA Queens ya Uganda imemaliza kwa kishindo mechi ya Kundi A kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake CECAFA baada ya kuichapa Denden FC ya Eritrea mabao 7-0 mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyayo Nairobi, Kenya.
Mechi ya kwanza Kampala ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya wenyeji wa mashindano hayo, Police Kenya ambayo ina mechi moja mkononi.
Mabingwa hao wa Ligi ya Wanawake Uganda, walitumia dakika nne tu tangu kuanza mechi hiyo kuandika bao la kwamza kupitia, Kamiyati Naigaga akimalizia krosi safi iliyozua shangwe kwa mashabiki uwanjani na dakika 55 baadae akafunga la pili.
Wachezaji wengine waliofunga mabao ya washindi ni; Tourist Lema aliyeweka mawili dakika ya nane na 47, Peace Muduwa aliyefunga dakika ya 32, 46 na Zaituna Namaganda aliyekamilisha idadi hiyo dakika 77.
Ushindi huo unaifanya Kampala kusogea hadi nafasi ya kwanza ikiwa tayari imemaliza mechi zote mbili za kundi A ikiwa na pointi tatu sawa na Police Kenya iliyoko nafasi ya pili na mechi moja mkononi.
Licha ya ushindi huo, lakini Kampala bado haijafuzu kucheza nusu fainali ikisikilizia matokeo ya mechi ya mwisho kati ya Police dhidi ya Denden.
Kama Police itapata ushindi mechi ya mwisho au sare yeyote itavunja matumaini ya Kampala kufuzu hatua hiyo kwani timu moja iliyokusanya pointi nyingi kwa kila kundi inakwenda hatua inayofuata.