Murang’a Seal wanafukuza ubingwa kimya kimya

HUU ni msimu wao wa kwanza wanakipiga Ligi Kuu Kenya na baada ya mechi 10, Murang’a Seal wapo kwenye mix mbio za ubingwa.

Chini ya kocha mzoefu Gabriel ‘Kingi’ Njoroge aliyechukua mikoba ya Vincent Nyaberi ambaye alihusika pakubwa kuipandisha daraja Murang’a Seal, timu hii yenye maskani yake Kaunti ya Murang’a ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa FKFPL wakiwa na pointi 20.

Wanakabana koo kwa pointi na mabingwa watetezi Gor Mahia ambao hata hivyo wapo nafasi ya pili kutokana na ubora wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku wakizidiwa pointi moja na Posta Rangers.

Mambo yanaweza yakabadilila wikendi hii na Murang’a Seal wakajikuta kileleni mwa ligi hiyo ambayo ndiyo yenye hadhi humu nchini endapo watawafunga Gor Mahia na kisha AFC Leopards iwafanyie ‘favour’ kwa kuwafunga Rangers.

Hayo tuyawache kwa wikendi inayokuja, ila mwishoni mwa wiki iliyopita, vijana wa Njoroge walipunguza wigo wa pointi na vinara wa FKFPL kufuatia ushindi mtamu dhidi ya mabingwa wa zamani Tusker FC wakati Rangers na Gor Mahia wakibanwa kwenye ngarambe zao.

Murang’a Seal sio timu inayoongelewa sana hususan kwenye mbio za ubingwa FKFPL ila kwa jinsi kocha Njoroge alivyokisuka kikosi chake, wanaweza kurudia historia iliyowekwa na Sofapaka FC mwaka 2009 ambapo walichukua ubingwa wa ligi katika msimu wao wa kwanza.

Mechi dhidi ya Gor Mahia wikendi hii ni mtihani kwao kudhibitisha wanautaka ubingwa lakini tayari msimu huu licha ya kutoka nyuma na kuwafunga Tusker FC mabao 2-1, waliwapiga pia washindi wa Mozzart Bet Cup na wawakilishi pekee michuano ya kimataifa, Kakamega Homeboyz, bao 1-0 tena ugenini.

Presha ambayo Muranga’a Seal wanayowapa timu zinazowania ubingwa FKFPL msimu huu ndiyo presha waliyonayo Rangers kudhihirisha hawapo kileleni kwa bahati tu.

Rangers inayofundishwa na John Kamau imekua na mwanzo mzuri wa msimu ila mechi zao mbili za mwisho zimemalizika kwa sare na juzi walitoka 0-0 na KCB ikiwa ni siku tatu tu baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Homeboyz.

Hata hivyo, kocha Kamau yuko relax kwasababu anaamini hali hiyo kimchezo ni kawaida na haitadumu sana watarudi kwenye mstari wao wakilenga zaidi ubingwa.

“Bado hatujacheza na wapinzani wetu wa karibu, Gor Mahia, hii ikimaanisha tunayo pointi sita za kuzipigania,” alisema kocha huyo wa Rangers na kuongeza ligi itakosa mvuto kama kinara kwasasa atawaacha wenzake kwa wingi wa pointi.