MULEE: KOMBE LA DUNIA TU? TULIENI

KOCHA wa Harambee Stars, Jacob Ghost Mulee sasa kaelekeza nguvu zake kwenye mechi za kufuzu kushiriki kombe la dunia 2022.
Hii ni baada ya Star kuchujwa kwenye kinyang’anyiro cha kufuzu kwa dimba ka AFCON 2022 baada ya kutoka sare ya 1-1 na Misri Alhamisi iliyopita.
Mulee ambaye kwa sasa yupo kwenye mchakato wa kukisuka kikosi kipya kabisa cha Harambee Stars kasema mipango yake sasa ipo kwenye World Cup qualifiers.
“Kwa sasa tuna picha nzuri ya aina gani ya ushindani tunaopaswa kutarajia kwenye mechi za kufuzu kushiriki kombe la dunia. Tupo kwenye kundi linalowajumuisha Mali, Rwanda na Uganda na tunafahamu haitakuwa rahisi. Lakini kwa utathmini wa jinsi tunavyoendelea kukisuka kikosi kipya, kuna uwezekano tutapenyeza na kufuzu.” Mulee anasema.
Baada ya mchuano wa Togo, Mulee pia anataka kupangiwa mechi kadhaa za kirafiki anapoendelea na mchakato wake wa kuivisha Stars mpya.
“Tukipata mechi za kirafiki na wapinzani dhabiti, itatusaidia hata zaidi kubusti morali yetu na imani kwekwenye uwezo wa wachezaji wetu.” Anasema.
Aidha Mulee kawasifia wachezaji wanaosakata soka lao kwenye ligi ya nyumbani waliopata nafasi ya kucheza kwenye kikosi chake na hawakumwangusha.
“Nimeishi kusisitiza hapa kwamba ligi kuu ya Kenya ina ushindani mkubwa na sio lazima kila siku tuwategemee wachezaji wa majuu. Nafikiri hilo sasa limedhibitika na kila mmoja kajionea kutokana na matokeo ya wachezaji wa ndani tuliowapa fursa. Lakini pia hii ni kuwapa imani tu wachezaji wa ndani kwamba kupata namba kwenye timu ya taifa sio kazi ngumu ilmuradi unajituma. Sio lazima upate ulaji nje ya nchi ndio eti upate namba kwenye timu ya taifa.” Mulee kaongeza.
Sifa za kocha huyo zimeewaendea wachezaji watatu wa ndani wing’a wa Bandari Abdallah Hassan, fulu beki wa kulia anayeichezea Kariobangi Sharks Dan Sakari na beki wa kati anayekipiga Wazito FC Johnstone Omurwa.