Muguna: naondoka Gor

Muguna: naondoka Gor

What you need to know:

  • KIUNGO fundi wa Harambee Stars Kenneth Muguna kadhibitisha hana mpango wa kuendelea kuichezea Gor Mahia na tayari kabadilisha agenti wake kwenye harakati zake za kusaka klabu mpya.

KIUNGO fundi wa Harambee Stars Kenneth Muguna kadhibitisha hana mpango wa kuendelea kuichezea Gor Mahia na tayari kabadilisha agenti wake kwenye harakati zake za kusaka klabu mpya.

Muguna aliyepokonywa unahodha wa Gor kutokana na kile kinachoaminika kuvunjika kwa mahusiano kati yake na uongozi wa klabu, kwa sasa anaripotiwa kuwa kwenye rada za klabu kadhaa.

Miamba wa soka kutoka DR Congo DC Motema Pembe, miamba wa soka Angola, Petro Atletico na wazito kwenye ligi kuu ya Tanzania, Simba SC na Yanga SC wote wameripotiwa kuwa kwenye rada ya kiungo huyo mbunifu.

Ili kuweka mambo yake sawa, Muguna kaamua kusaini na ajenti tofauti anayeamini atamwezesha kuangukia dili safi ili aweze kujitoa Gor.

“Sasa hivi nina wakala mpya baada ya mkataba wangu na yule wa awali kumalizika na nikaamua sitairefusha tena naye. Kwa sasa sitamtambulisha hadharani ila ni jamaa ambaye kawashughulikia wachezaji kama (Modou) Barrow na (Ogenyi) Onazi. Kuanzia dirisha lijalo la usajili, ndiye atakayenishughulikia.” Kasema Muguna.

Kiungo huyu ambaye kwa sasa anauguza jeraha baada ya kuumia akiicheza Stars dhidi Misri alikoonyesha kiwango, anasema suala la fedha na ubora wa ligi husika ndizo vigezo atakavyozingatian kabla ya kufanya maamuzi ya klabu mpya atakayojiunga nayo.

Muguna mwenye miaka 25, kwa mara nyingine tena msimu huu ameonekana kuibeba Gor akihusika kwenye magoli kumi kabla ya ligi kusitishwa. Kapachika manne na kutoa asisti sita.