Mfukoni Ingwe safi, dimbani mmh!

New Content Item (3)

MABINGWA wa zamani Ligi Kuu Kenya, AFC Leopards bado wanasubiri ushindi wao wa kwanza msimu huu wakijikuta katika nafasi ya 15 na pointi nne tu kwenye msimamo baada ya kushuka dimbani mara tano.

Licha ya matokeo kuwakalia vibaya, Ingwe wamekuwa wakinufaika na mapato yatokanayo na malipo ya viingilio vya mechi.

Takwimu za msimu uliopita zilizotolewa na Shirikisho la Soka Kenya (FKF) zilionyesha Ingwe ndiyo iliyoongoza kwa mafans wake kujitokeza kwa wingi uwanjani japo hawakushinda taji lolote tofauti na watani zao Gor Mahia waliyotwaa ubingwa wa 20 FKF-PL.

Kwa kiasi kikubwa, aliyekuwa Kocha mkuu, Patrick Aussems alichangia hamasa ya mafans wa Ingwe kujitokeza kwa wingi uwanjani iwe ni gemu za nyumbani au ugenini msimu uliopita na alikuwa na utaratibu wa kutumia mtandao wa kijamii kueleza yaliyo ya moyoni kuhusu timu, uongozi, wachezaji, marefa na mafans.

Msimu huu, Leopards wanaonekana kupata compe kutoka kwa Shabana FC ambayo mafans wao wamekuwa wakiifuata timu yao popote walipo ikiwemo kujitokeza kwa wingi wanapocheza Uwanja wa Raila Odinga uliyopo Kaunti ya Homabay gemu zao za nyumbani baada ya kufungwa uga wa Gusii, Kaunti ya Kisii kwa ajili ya ukarabati.

Hadi sasa, Leopards wameshacheza michezo mitatu ya nyumbani wakifanikiwa kuvuna kiasi cha Sh 2,259,900 inayotokana na viingilio vya getini kwenye viwanja vitatu tofauti walivyovitumia.

Mwishoni mwa wiki iliyopita wakicheza ugani Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi katika mechi dhidi ya Shabana, Leopards walitangaza kukusanya Sh1,426,300 ikiwa ni mauzo ya tiketi za kielektroniki.

Hadi sasa hii ni idadi kubwa ya mafans kuhudhuria mechi za FKFPL ambapo jumla ya tiketi 6,152 ziliuzwa na kushuhudia jukwaa la kawaida Ingwe ikivuna Sh1,099,800 kutokana na tiketi moja kuuzwa Sh200 na Sh326,500 kukasanya jukwaa la VIP tiketi moja ikiuzwa kwa Sh500.

Katika mechi ya kwanza msimu mpya, Leopards walicheza na FC Talanta kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi na walifanikiwa kukusanya Sh615,700 kutokana na mauzo ya tiketi na jumla ya mashabiki waliojitokeza walikuwa 3002.

Mapato yao yalipungua zaidi walipocheza na Muhoroni Youth kwenye Uwanja wa Kimataifa Moi Kasarani jijini Nairobi wakikusanya Sh217,900 kutokana na mashabiki 1,028 waliohudhuria mtanange huo ikidaiwa uchache wa mashabiki ulitokana na matokeo yasiyoridhisha.

Hata hivyo, Ingwe ambao watakuwa wenyeji katika Mashemeji Derby wikendi hii, wanatarajia kuvuna kiasi kikubwa cha fedha kutoka mapato ya viingilio ikizingatiwa wanatumia mfumo wa e-ticketing inayopunguza msururu mrefu na msukumano wa watu kupata tiketi wakati wa mechi.