Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

McCarthy: Tulichokutana nacho Burundi haikuwa mechi ya soka ni vita

Benny Pict

Muktasari:

  • McCarthy amesema katika mechi hiyo ya Kundi F iliyochezwa Oktoba 9, 2025 kwenye Uwanja wa Intwari nchini Burundi, wapinzani wao walijaribu kuigeuza mechi hiyo kama vita badala ya kuonyesha ustadi na mchezo wa kiungwana.

Kocha Benni McCarthy, amesema kikosi chake cha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, hakikutekeleza vyema mpango waliouweka katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 dhidi ya wenyeji wao Burundi, kwa sababu wapinzani wao walicheza kwa ubabe sana.

McCarthy amesema katika mechi hiyo ya Kundi F iliyochezwa Oktoba 9, 2025 kwenye Uwanja wa Intwari nchini Burundi, wapinzani wao walijaribu kuigeuza mechi hiyo kama vita badala ya kuonyesha ustadi na mchezo wa kiungwana.

“Burundi walicheza kwa ukatili sana, na waliruhusiwa kufanya mambo mengi bila kuchukuliwa hatua. Hawakuwa wanacheza kandanda. Walicheza kana kwamba walitaka kuvunja miguu ya wachezaji wetu. Sikuja Burundi kushuhudia aina hii ya soka,” amesema.

Aliongeza kuwa uwanja wa nyasi bandia wa Intwari wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 22,000 haukuwasaidia Wakenya, ambao walishinda 1-0 dhidi ya The Swallows.

Kutokana na changamoto hizo, gwiji huyo wa soka kutoka Afrika Kusini aliuelezea ushindi huo mgumu kama haki ilitendeka dhidi ya wenyeji wao.

Bao pekee la Harambee Stars lilifungwa dakika ya 73 na mshambuliaji Ryan Ogam aliyetokea benchi na kuifanya Kenya kupata ushindi wa pili ugenini kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026. Kabla ya hapo iliichapa Shelisheli mabao 0-5, Novemba 20, 2023.

“Hatujazoea kucheza kwenye uwanja wa aina hii. Tangu mwanzo lilikuwa jambo gumu sana kwetu,” McCarthy alisema baada ya mechi.

“Najivunia sana wachezaji wangu kwa kuonyesha ari na ujasiri katika mazingira magumu mno. Tumeonyesha tabia ya ushindani na dhamira ya kweli. Tumethibitisha kwamba sisi ni taifa lenye soka bora.”

“Kwangu, kile ambacho timu ya taifa ya Burundi ilionyesha haikuwa kawaida. Lakini haki imetendeka. Ushindi huu ni wa ajabu.”

Katika mechi hiyo, mapema dakika ya pili, kipa Brian Bwire alilazimika kuondolewa uwanjani baada ya kuumia kichwani kufuatia kugongwa na Caleb Bimenyimana wa Burundi aliyekosa mpira na kumkanyaga. Bimenyimana alionyeshwa kadi nyekundu, na Kenya ikamwingiza kipa Byrne Odhiambo kuchukua nafasi yake.

McCarthy amesema Bwire alipata jeraha la sentimita 12 (inchi tano) juu ya jicho na kumkosoa mchezaji wa Burundi kwa rafu hiyo.

“Kama mshambuliaji, unatakiwa kwenda kwenye mpira, lakini kama unagundua hutaufikia, kwa nini uinue mguu hivyo?” amehoji.

Aliongeza kuwa baada ya jeraha hilo la mapema, wachezaji wake waliogopa kucheza kwa uhuru wakihofia kuumia pia.

“Ilikuwa ngumu sana kwa sababu wachezaji wangu walikuwa na hofu ya kujeruhiwa kama wenzao.”

Nahodha Michael Olunga naye alikubaliana na maneno ya kocha wake aliposema: “Ilikuwa mechi ngumu, hasa kutokana na hali ya uwanja na joto. Ni sawa kuwa na mchezo wa nguvu, lakini si wa ukatili. Hatukuufurahia mchezo, lakini tunashukuru kwa ushindi.”

Hata hivyo, Kenya haikuweza kutumia vyema faida ya kucheza na mchezaji mmoja zaidi, na ilianza kuonekana imara zaidi kipindi cha pili baada ya Timothy Ouma kuchukua nafasi ya Vincent Harp.

Tangu Machi, Harambee Stars imekuwa ikicheza mechi zake za nyumbani kwenye viwanja vya nyasi asilia vya Moi International Sports Centre na Uwanja wa Taifa wa Nyayo.

Kocha wa Burundi, Patrick Sangwa, amesema hakuwa na cha kufurahia, kwani malengo yao yalikuwa kupata ushindi.

“Burundi tulitaka ushindi, lakini bahati haikuwa upande wetu. Sijafurahishwa, lakini tumecheza vizuri,” amesema Sangwa.

Hata hivyo, timu hizo zote hazina nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia, michuano itakayofanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwaka 2026, ikiandaliwa kwa pamoja nchi za Canada, Marekani na Mexico, ambapo mataifa 48 yatashindana kuwania ubingwa wa dunia.

Kenya inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12, wakati Burundi ni ya tano na pointi zake 10. Kinara wa kundi ni Ivory Coast (23) ikifuatiwa na Gabon (22). Shelisheli inaburuza mkia haina pointi, Gambia ni ya nne ikikusanya pointi 10.

Kesho Jumanne Oktoba 14, 2025, timu zote za kundi F zitakuwa uwanjani kumalizia mechi moja ya mwisho kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 ambapo ratiba ipo hivi; Shelisheli vs Gambia, Gabon vs Burundi na Ivory Coast vs Kenya.