MATANO AWAPA TANO VIJANA WAKE KWA USHINDI

Wednesday June 23 2021
MATANO PIC
By John Kimwere

KOCHA wa Tusker FC, Robert Matano ameelezea furaha yake kutokana na ushindi wa vijana wake wa bao 1-0 dhidi ya Kariobangi Sharks kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Betking Kenya Premier League (BKPL) msimu huu.

Tusker ilishuka dimbani kushiriki patashika hiyo ikiumiza majeraha ya kushindwa mara mbili. Wana mfinyo hao walikuwa wamegongwa bao 1-0 na AFC Leopards kwenye mechi ya kuwania Betway Cup pia walizabwa bao 1-0 na Posta Rangers kwenye mchuano wa ligi.

''Kusema ukweli tulihitaji ushindi wa alama zote tatu bila kujali tuliupata namna gani bora tulizima wapinzani wetu na kutia kapuni pointi tatu muhimu,'' kocha huyo alisema na kuongeza kuwa katika kipindi cha kwanza vijana wake walipoteza nafasi nyingi wangezitumia kunyamazisha wapinzani wao.


Veterani huyo anasema bado anaumizwa na kichapo cha Posta Rangers maana kiliwanyima nafasi ya kupanua mwanya katika jedwali la kipute hicho. Kocha huyo anashikilia kuwa hadi sasa haelewi jinsi walivyokubali kuchapwa na Posta Rangers.

Matakeo mbaya ya Tusker FC,  AFC Leopards na KCB yamechangia mabingwa watetezi, Gor Mahia kupiga hatua zaidi ambapo imetinga kati ya tatu bora huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi. Katika jedwali, Tusker inaongoza kwa kutia kapuni alama 42, moja mbele ya KCB baada ya kila moja kushiriki mechi 20. Gor Mahia imefunga tatu bora kwa alama 37 sawa na mashameji wao AFC Leopards.


Advertisement
Advertisement