MASHEMEJI GOR, AFC LEOPARDS WAIPIGA VITA FKF-PL

Thursday November 18 2021
vita pic
By Sinda Matiko

MARA tu baada ya serikali kupindua utawala wa Rais wa FKF, Nick Mwendwa, viongozi wa Gor na mashemejio AFC wameanza kuipiga  vita ligi ya FKF-PL
Timu zote hizi zinashiriki ligi hiyo ambayo imekuwa ikiendeshwa na FKF  toka msimu uliopita.
FKF ilichukua usukani wa kuendesha ligi wenyewe baada ya mkataba wao na kampuni ya Kenya Premier League (KPL) kumalizika.
Utakumbuka kuwa kampuni ya KPL  ilikuwa na mkataba wa kuendesha ligi kuu nchini kwa niaba ya FKF. Mkataba huo ulifika kikomo Septemba mwaka jana na FKF ikadinda kuurefusha na baadala yake kuamua itajiendeshea ligi yenyewe.
Uamuzi huu ulitokana na  tofauti zilizoshuhudiwa kati ya Mwendwa na KPL kuhusu namna ya usumamizi wa ligi hiyo.
Kwa mfano Februari 2016, mara tu Mwendwa alipochaguliwa, alishinikiza ligi ipanuliwe kutoka timu 16 hadi 18. KPL walipinga huku FKF iking'ang'aniza. Mwisho wa siku FKF ilipata baraka za FIFA kupanua ligi hiyo. Kilichofuatia ni wadhamini wakuu  Supersport kufuta udhamini wao wa mamilioni ya pesa. Aidha wadhamini wengine walifuata mkondo. Nyongeza za timu ilikuwa na maana kuwa gharama ingepanda na wadhamini hawakju tayari kuongeza fedha zaidi ya kile walichokuwa wkaitoa. Chini ya Mwendwa ligi ya FKF-PL imeshindwa kuvutia udhamini wa maana.
Sasa viongozi wa Gor wanaamini kuwa njia ya pekee ya kuwarejeshwa wadhamini kwenye ligi kuu ya Kenya pamoja na ushindani uliokuwepo zamani, ni kurejesha usimamizi wa ligi kwenye mikono ya kampuni kibinfasi kama ilivyokuwa na KPL.
"Kamati Shikilizi iliyopo madarakani kwa sasa inapaswa kuipa majukumu ya uendeshaji wa ligi kuu kampuni ya kibinfasi iwafanyie shughuli hiyo kwa niaba yao. Hivi hata klabu zitapata fursa ya kuchangia kwenye maamuzi. Ndivyo ilivyokuwa wakati wa KPL. Hayo yalibadilika FKF ilipochukua usukani. Klabu tulikosa uhuru wa kuchangia mawazo au kukosoa mambo kadhaa. Ndio sababu uhusiano wa klabu na FKF ulidorora." anasema Ambrose Rachier mwenyekiti wa Gor.
Ni mtazamo anaokubaliana nao mwenyekiti wa Ingwe, Dan Shikanda mia fil mia.
"Sio lazima iwe kampuni ya KPL ila tunaweza kutumia mfumo waliokuwa wakiutumia na ulikuwa ukifanya kazi vizuri sana. Kamati inayoundwa na wenyekiti wa klabu ndio inayopaswa kuwa ikiendesha ligi kuu. Hivi hata haya malalamishi m ya marefa kuwa na mapendeleo kwenye mechi, yataisha sababu kwa sasa hilo ni mojawepo ya changamoto kubwa tunayokabiliana nayo." anasema Shikanda.
Mitazamo ya mabazuu hao imepigwa jeki vile vile na mdosi wa Posta Rangers, John  Tanui.
"Uwepo wa bodi huru kama kampuni ya kibinfasi kwenye uendeshaji wa ligi kuu utasaidia sana kuzuia FKF kujaribu kuvuruga mambo suala ambalo tumelishuhudia sana toka msimu uliopita." Tanui anasema.
Gor na Ingwe wameshawahi kukwaruzana na utawala wa Mwendwa mara si moja. Julai mwaka huu timu hizo zilisusia  mechi ya ligi kuu ya Mashemeji Derby  baada ya FKF kukayagia kuwalipa pesa zao za kombe la Betway Cup. Gor na Ingwe walifika fainalini na hata baada ya mchuano huo, walilazimika kusubiri zaidi ya miezi minne kulipwa.
Mwendwa alijibu mapigo kwa kuzipiga fainio ya Sh10 milioni klabu hizo na pia kuwapokonya alama tatu kila mmoja.
Aidha Rachier na Shikanda walipigwa marufuku ya kujishughulisha na masuala yeyote ya soka yanayohusu FKF.

Advertisement