Mashabiki Mombasa waifuata Kariakoo derby

WIMBI la mashabiki wa soka kutoka Mombasa wanaelekea Bongo kushuhudia mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga ambayo imekua gumzo humu nchini.
Mechi hiyo ambayo itapepetwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Jumapili imewavutia mashabiki ambao wameanza kuondoka Mombasa tangu Alhamisi kwa kutumia magari madogo pamoja na mabasi.
Mmoja wa maofisa wa kampuni ya mabasi ya Tawakal yanayofanya safari zake kutoka Mombasa kwenda Dar, Mudrick Mohamed Kassim, alisema amepokea wasafiri hususan vijana ambao wameondoka kuelekea Bongo kwa ajili ya mechi hiyo kubwa ukanda huu wa Afrika Mashariki.


“Siku ya Alhamisi tumekuwa na vijana wengi walioondoka nikiwa nawasikia wakisema wanaelekea huko (Dar) kucheki mechi ya Yanga dhidi ya Simba. Ni uhakika tangu Alhamisi na Ijumaa tumepokea abiria wengi na ya kesho (leo) Jumamosi tumekaribia kujaza,” alisema Kassim.
Naye mwenzake wa mabasi ya Tahmeed, Jaffer Suleiman, alisema kumekuwa na ongezeko ya abiria wanaoelekea Dar kwa siku tatu mfululizo ya hivi karibuni akihusisha ongezeko hilo na mechi hiyo bab’ kubwa ambayo Mkenya Joash Onyango anatarajiwa kucheza akiitumukia Simba.
Moja wa kiongozi wa mashabiki wa Simba kutoka Mombasa ambaye yupo safarini kuelekea Bongo, Abdillahi Ali, aliambia MWANASPOTI kuwa yeye pamoja na wenzake 10 waliondoka kwa magari madogo matatu usiku wa Jumatano.
“Hii sio mechi ya kukosa wala kusimuliwa, nataka kuishuhudia kwa macho yangu mwenyewe Simba ikiwashinda watani zetu Yanga,” alisema Ali.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kaunti ya Mombasa (MCFA), Juma Alliy Goshi, naye alisema anaondoka leo Jumamosi kwa basi kuelekea Dar kuishangilia timu yake ya Simba akiongeza alikuwa aondoke na wenzake kwa usafiri wa gari lake lakini wamekosa ruhusa makazini kwao.