Mafans 8,000 kuicheki Stars

KIKOSI cha timu ya taifa, Harambee Stars, kimekita kambi nchini Uturuki kikiendelea kunoa makali chini ya kocha Engin Firat tayari kuwakabili waliyokuwa wenyeji wa Kombe la Dunia 2018, Urusi.

Mechi hii ya kimataifa ya kirafiki ambayo ina umuhimu katika Kenya kuboresha viwango vyake vya ubora wa soka vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) itachezwa Jumatatu Oktoba 16 ugani Titanic Mardan uliyopo jijini Antalya.

Uwanja huu wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 7,938 ulijengwa ndani ya mwaka moja kuanzia 2007 hadi 2008 na unatumika kwa mazoezi na mechi za majaribio na klabu ya Antalyaspor inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki.

Mwaka 2008, uga huo ulitumika kuandaa michuano ya Ulaya chini ya miaka 17 ikiwemo mchezo wa fainali ambapo Hispania iliitembezea Ufaransa kichapo cha mabao 4-0.

Hii itakua mara ya kwanza Harambee Stars inacheza dhidi ya Urusi ambapo kwenye viwango vya FIFA, Kenya ni ya 109 wakishuka nafasi nne wakati Urusi walishuka nafasi moja na sasa wapo 39.

Kuelekea mechi hiyo, kocha Firat alieleza kuhusu kukosekana kwa beki Daniel Anyembe anayekipiga na Viborg ya Denmark akisema klabu yake imekuwa wazito kumuachia.

Beki huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 25, amecheza mechi tatu na alikuwa moto pasi Stars ikiichapa Qatar mabao 2-1.

“Tulitaka tuwe na Anyembe kwenye kambi, lakini klabu yake wamekuwa wagumu kumuachia. Tumeshawasiliana nao (klabu ya Viborg) na tunaimani tutakua naye hapa tayari kwa mechi yetu ya Jumatatu,” alisema kocha Firat.

Wakati Firat akimsubiri Anyembe ambaye baba yake mzazi ni Mkenya na mama yake ni raia wa Denmark, kocha wa Urusi Valery Karpin amewajumuisha Alexander Golovin anayekipiga na Monaco ya Ufaransa, Daler Kuzyaev wa Le Havre pia ya Ufaransa na Alexei Miranchuk anayechezea Atalanta ya Italia.

Urusi wanaivutia kasi Stars kwa kucheza na Cameroon leo Alhamisi kwenye dimba la Dynamo jijini Moscow.