KPA, GSU zatinga robo fainali CAVB

WASHIRIKI wapya timu ya Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) na General Service Unit (GSU) kila moja ilionyesha uwezo wake na kujikatia tiketi ya robo fainali kwenye mechi za Voliboli ya Klabu Bingwa Afrika (CAVB) inayoendelea jijini Tunis, Tunisia. Timu hizo kila moja ilishinda mechi mbili na kupoteza moja. KPA chini ya kocha, Sammy Mulinge ilizaba Army Patriotigue Rwandaise (APR) ya Rwanda seti 3-2  kwenye mechi za Kundi  A kabla ya kunyukwa na Esperance ya Tunisia seti 3-0 kisha kumaliza mechi za mchunjo vizuri kwa kuzoa seti 3-0 mbele ya Rukinzo ya Burundi. Nao madume wa GSU chini ya kocha, Gideon Tarus waliokuwa wamepangwa Kundi D, walianza vibaya walipolazwa seti 3-0 na  Zamalek ya Misri. Hata walifanikiwa kulipiza kisasi kwa kushinda Nigeria Customs ya Nigeria 3-1 kisha kubeba seti 3-0 mbele ya Espoir ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.    
''Nashukuru wachezaji wangu kwa kujituma kwenye kampeni zetu licha ya kwanza ndio mwanzo kushiriki kipute hicho,'' kocha wa KPA alisema na kuwataka vijana wake kujitahidi kiume kwenye mechi ya robo fainali.
 Naye kocha wa GSU alisema ''Kuteleza sio kuanguka bado tumepania kumaliza kati ya nne bora kwenye ngarambe ya mwaka huu.''
 Kwenye matokeo mengine, Kundi D, Zamalek ya Misri iliomaliza kifua mbele baada ya kuzaba GSU, iliangusha Espoir ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa seti 3-0 kisha kutia kapuni seti 3-0 dhidi ya Nigeria Customs ya Nigeria.