Kocha Gor atoboa siri ya mafanikio

JOHNATHAN McKinstry amedai sababu ya matokeo mazuri ya kikosi chake hadi sasa imechangia pakubwa na ki-smart.

Kwa muda mrefu, miamba hawa wa soka nchini walitawala Ligi Kuu Kenya hadi misimu miwili iliyopita walipopoteza dira na kupokonywa taji na Tusker FC.

Ila msimu huu, Gor wameonekana kurudi kwenye makali yao ya zamani wakiwa wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa alama 24 wakizidiwa alama tatu na vinara Nzoia Sugar japo wamecheza mechi mbili zaidi ya Gor.

Katika mechi 11 walizocheza, K’Ogalo wamepoteza mara moja tu, kutoka sare tatu na kusajili ushindi mara saba.

Lakini licha ya kasi nzuri hiyo, kocha McKinstry anasisitiza sababu kubwa ambayo imewababa hadi sasa ni kuwa wamekuwa wakiangukia bahati kwenye mechi zao.

“Tupo kwenye mbio za ubingwa kwasababu ya bahati nzuri. Nasema hivi kwasababu kikosi nilichonacho ni cha wachezaji 18 tu. Ni kikosi finyu sana ukizingatia bado tunatumikia marufuku ya FIFA ya kutosajili,” alisema kocha huyo raia wa Ireland Kaskazini.

Ni kwasababu hii, McKinstry anasema kama ikitokea washinde kombe, basi itakuwa mojawepo ya rekodi zake bora zaidi.

“Unapokuwa na kikosi kidogo kama hicho, huwezi kushindana vizuri sababu yakitokea majeraha umekwisha. Ndio maana nasema ni bahati sababu tumebahatika kuepuka kuwa na wachezaji majeruhi mpaka sasa na hiyo imetusaidia sana,” ameongeza timu hiyo ikiikabili Nairobi City Stars leo Jumamosi.