Kocha Gor abambika na watoi

MKUFUNZI mpya wa Gor Mahia, Johnathan McKinstry anawazia kuwaacha nje ya kikosi chake cha kwanza wachezaji wazoefu ili kutoa fursa kwa watoi waliombamba.

Mwezi uliopita Gor iliwasimamisha kwa muda wa wiki mbili wachezaji 10 wanaounda kikosi chao cha kwanza kwa kile walichokitaja utovu wa nidhamu.

George ‘Blackberry’ Odhiambo, Austin Odhiambo, John Ochieng, Boniface Omondi, Ernest Wendo, Benson Omanyala, Sydney Ochieng, Dennis Ng'ang’a na Alpha Onyango ni miongoni mwa waliyosimamishwa na uongozi wa klabu baada ya kususia vikao vya mazoezi wakilalamikia mishahara yao.

Hata hivyo, wachezaji hao walirejeshwa kikosini lakini katika kipindi ambacho hawakuwepo, kocha McKinstry alilazimika kuwapandisha ngazi baadhi ya wachezaji wa kikosi chipukizi cha klabu.

Licha ya kurejea kwa mastaa hao, Mckinstry kakiri wazi wazi kwamba ana mpango wa kuwachuja baadhi ya wachezaji hao ili kutoa nafasi kwa wachezaji watoi waliombamba.

“Kusema kweli tunazidi kuboreka kila kukicha. Mechi hizi za kirafiki ni dhibitisho kuwa tunazidi kuiva. Ukiwangalia wachezaji tuliopromoti kutoka timu chipukizi, wanazidi kuiva na kwa misingi hiyo, baadhi yao watasalia kwenye kikosi cha kwanza ili wazidishe ushindani. Kwasasa hakuna mwenye uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza,” alisema McKinstry baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya KCB waliyolimwa 2-1.

Gor wamefungiwa kufanya usajili na FIFA hadi Januari mwakani baada ya kushindwa kuwalipa fidia wachezaji wao wa zamani waliowavunjia mikataba bila ya kufuata utaratibu unaostahili.