Kocha Batoto Ba Mungu awaza kimataifa

KOCHA mkuu wa Sofapaka FC, David Ouma, amepania kuongoza klabu hiyo kucheza michuano ya Afrika ngazi ya klabu.
Mara ya mwisho Sofapaka maarufu Batoto Ba Mungu kukipiga kimataifa ilikuwa mwaka 2014 katika michuano ya CAF Confederation Cup baada ya kushinda Kombe la FKF lakini walishindwa kutinga hatua ya makundi kufuatia kufungwa na FC Platinum.
Ouma ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake, Harambee Starlets, alisema kucheza kimataifa ni mojawapo kati ya malengo yake kwenye kampeni za FKFPL msimu mpya.
“Kwenye kampeni za msimu uliyopita tulikuwa na wakati mzuri lakini muhula huu lazima tujiwekee malengo muhimu kwa kuzingatia Sofapaka ni kati ya klabu kubwa hapa nchini,” alisema kocha huyo wa mabingwa 2019.
Ouma alisema kwasasa ana kikosi thabiti ambacho kimeiva tayari kupiga shughuli japo wapo baadhi ya wachezaji wanauguza marejuhi.