Kisa tukio la kuotea, mwamuzi Kenya ashushwa daraja
Muktasari:
- Taarifa ya FKF, imesema mwamuzi msaidizi wa pili, Jackson Opiayo, ameshushwa daraja kutokana na uamuzi wake tata kwenye mechi hiyo iliyochezwa Novemba 9, 2025 katika Uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF), limetangaza adhabu ilizochukua za makosa ya kinidhamu dhidi ya maofisa watatu kufuatia mapitio ya Kamati ya Waamuzi Taifa kuhusu Mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) Namba 68 kati ya Kakamega Homeboyz FC na Murang’a Seal FC.
Taarifa ya FKF, imesema mwamuzi msaidizi wa pili, Jackson Opiayo, ameshushwa daraja kutokana na uamuzi wake tata kwenye mechi hiyo iliyochezwa Novemba 9, 2025 katika Uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Katika taarifa hiyo, shirikisho hilo limesema Opiayo atapangiwa kushiriki mechi za National Super League (Ligi Daraja la Kwanza) kwa raundi tatu baada ya kutoa uamuzi usio sahihi wa kuotea kutokana na nafasi yake mbaya uwanjani.
“Hatua hii inafuatia uamuzi wa kuotea uliotolewa kutokana na kupangika vibaya, uliokosesha timu iliyoshambulia nafasi halali ya kupata bao. Utendaji wake wakati wa majukumu ya NSL utafuatiliwa kwa karibu, na ripoti ya kina itahitajika kabla ya kuzingatiwa kurejeshwa kwenye majukumu ya Ligi ya SportPesa,” imesema taarifa ya FKF.
Wakati huohuo, David Serem, aliyekuwa mwamuzi wa kati katika mechi hiyo, amepewa onyo kali baada ya kutoa uamuzi wa kona usio na msingi.
“Serem amepewa onyo kwa kutoa uamuzi wa kona bila sababu za wazi na bila ushauri wa kutosha kutoka kwa mwamuzi msaidizi. Kamati imebaini kuwa picha za video hazikuonyesha uthibitisho wa uamuzi wake, na maelezo aliyotoa wakati wa mapitio hayakutosha,” shirikisho limesema.
Pia, mwamuzi wa kwanza mwanamke, Gladys Kamuren, ameingia kwenye orodha ya wanaochunguzwa na shirikisho hilo akidaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, hivyo kuchangia uamuzi wa mwisho usio sahihi.
“Licha ya kuwa na nafasi nzuri ya kubaini kama mpira umetoka uwanjani, mawasiliano na ishara zake zilionekana kuwa hafifu na kuchangia kufikiwa kwa uamuzi usio sahihi,” shirikisho limeongeza.
FKF imesisitiza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya dhamira yake ya kuboresha ubora, uthabiti na uadilifu wa uchezeshaji katika mashindano yote inayoyasimamia, kupitia mafunzo endelevu, tathmini na hatua za marekebisho.
Hayo yanajiri wakati ambapo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa makocha wa ligi kuu kuhusu kuporomoka kwa ubora wa uchezeshaji.
Hivi karibuni, kocha wa Bidco United, Anthony ‘Vieira’ Akhulia, alimlaumu mwamuzi wa kati katika mechi yao dhidi ya Shabana iliyofanyika Jumapili katika Uwanja wa Gusii.
“Kwa kusema ukweli, uchezeshaji leo ulikuwa mbovu sana. Mwamuzi lazima atueleze ni kwa nini aliamua kutoa penalti kwa wapinzani wetu. Huu ni mtindo ambao tumeuona kwake... kwamba kila mechi ambayo Bidco inacheza, huwa anatoa uamuzi wa kutiliwa shaka,” alisema Akhulia.
Bidco ilipoteza mechi hiyo kwa bao moja pekee, jambo lililoiacha timu hiyo katika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 12.