Kipa Mkenya atoweka Zambia

MCHEZAJI wa kimataifa wa Kenya, Ian Otieno, bado hajarejea kwenye mazoezi ya Zesco United ya Zambia ikiwa inaingia siku ya 10 kulingana na kocha mkuu wa muda wa timu hiyo, Alfred Lupiya.

Kipa huyo wa zamani wa AFC Leopards aliwashangaza wengi katika mpambano wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya miamba wa Afrika Kusini, Royal AM, mchezo wa marudiano raundi ya pili.

Otieno alikusanya pasi ya nyuma ambayo ilisababisha mpira wa adhabu usio wa moja kwa moja uliowekwa wavuni na Ruzaigh Gamildien dakika ya 56 mpambano ukimalizika kwa sare ya bao 1-1 hivyo Zesco United kutolewa kwa sheria ya bao la ugenini kufuatia sare tasa nchini Afrika Kusini.

Kuondolewa huko kulimgharimu aliyekuwa kocha wao mkuu, Mumamba Numba, na kaimu kocha Lupiya alifichua bado hajamuona Otieno tangu sare dhidi ya Royal AM.