Kipa bora wa msimu Matasi awaruka Police

Thursday June 16 2022
kipa pic
By Sinda Matiko

NAIBU nahodha wa Tusker, Patrick Matasi aliyetawazwa kipa bora 2021/22 amekana ripoti zinazomhusisha na kuhamia  kwa makarao.
Matasi aliyejiunga na Tusker msimu huu, amekuwa katika fomu nzuri akiwaokolea sana mabingwa hao. Jitahada zake zilimpelekea kumaliza msimu akiwa na clean sheet nyingi zaidi ya kipa yeyote baada ya kutofungwa kwenye mechi 18.
Makarao Police FC ambao walipandishwa daraja msimu huu, walifanya usajili wa mastaa kibao kwa lengo la kutwaa ubingwa lakini hawakufanikiwa.
Mara tu baada ya Tusker kutawazwa mabingwa, tetesi zikazuka kuwa Police wameanza mchakato wa kutaka kumsajili kocha wa mabingwa hao Robert Matano na vile vile kipa Matasi.
Kocha Matano aliyecharuka na kutishia kujiondoa Tusker akidai hapewi heshima anayostahili, tayari amebadilisha lugha na kusema hatagura mpaka pale mkataba wake uliosalia na mwaka mmoja utakapofika kikomo.
Matasi naye amejitenga na tetesi za makarao, akisema kuwa angependelea kusalia na wategenezaji bia hao.
"Bado ningali na mkataba na Tusker na timu yeyote inayohitaji huduma zangu inafahamu vyema  utaratibu unaostahili kufuatwa. Hii ina maana kwamba ni lazima wafanye mazungumzo na Tusker ambao ndio waajiri wangu kwa sasa na ninawaheshimu," Matasi kawaruka makarao.
Matasi anasisitiza kuwa ana kila sababu ya kuwaheshimu Tusker hasa baada ya klabu hiyo kumsapoti sana alipohusika kwenye ajali  mbaya ya barabarani  miezi michache tu baada yake kuachana na St.Georges ya Ethiopia.

Advertisement