Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kigogo Homeboyz ataka Benni McCarthy atimuliwe

BENNY Pict

Muktasari:

  • Kipigo kibaya zaidi katika historia ya Kenya kilitokea mwaka 1961 ilipopoteza 13-2 dhidi ya Ghana katika mechi ya kirafiki ya kuadhimisha Siku ya Jamhuri. Wakati huo, Black Stars walikuwa na kikosi chenye nguvu kilichoongozwa na mshambuliaji hatari Ben Acheampong.

MWENYEKITI wa klabu ya Kakamega Homeboyz, Cleophas Shimanyula amelitaka Shirikisho la Soka Kenya (FKF), kumfukuza kocha wa timu ya taifa, Harambee Stars, Benni McCarthy kutokana na aibu ya kipigo cha mabao 8-0 ilichopewa timu hiyo na Senegal katika mechi ya kirafiki.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa Mardan Sports Complex, Antalya, Uturuki wababe Simba wa Teranga waliipasua Harambee watakavyo, kwani walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 6-0 kabla ya kuongeza mengine mawili baadaye.

Ikiongozwa na nyota wa zamani wa Liverpool, Sadio Mane, Senegal ilipachika mabao matatu ndani ya dakika 15 za mwanzo. Nyota anayecheza kwa mkopo Bayern Munich akitokea Chelsea, Nicolas Jackson alifungua karamu ya mabao dakika ya nane tu.

Senegal, iliongeza bao la pili kupitia El Hadji Malick Diouf, kisha Mane akafunga hat-trick kwa muda mfupi.

Katika kipindi cha pili, Senegal ilianza kwa Ibrahim Mbaye kutupia bao la saba kabla ya mtokea benchi, Cherif Ndiaye kupigilia msumari wa mwisho na kuwaacha vijana wa McCarthy wakiwa hoi na kutoka uwanjani wakiinamisha vichwa chini kwa aibu ya kipigo hicho kikubwa.

BEN 01

Kipigo hicho kimewafanya wadau wa soka wa Kenya kumjia juu kocha huyo raia wa Afrika Kusini, ambapo mmiliki wa Kakamega Homeboyz,  Simanyula alikaririwa na duru za kispoti zilizoripotiwa na Flashscore akisema: "Kocha wa kienyeji anaweza kufanya vizuri zaidi."

Kwa mujibu wa Shimanyula aliyekiri kuumizwa na kipigo hicho kikubwa, ni wakati muafaka kwa FKF kuangalia mbali zaidi ya gwiji huyo wa zamani wa klabu kadhaa barani Ulaya kuendelea kuwa kocha wa Harambee Stars.

“Ilikuwa kipigo cha kuumiza sana, hatujawahi kupoteza hivi kwa muda mrefu. Hatustahili kupoteza hivi, ilikuwa aibu,” Shimanyula amekaririwa na kuongeza:

“Kocha hakuwepo mazoezini (kabla ya timu kuondoka kwenda Uturuki), hakuwa karibu, na alikutana na timu akiwa tayari Uturuki. Je, kocha yuko makini na kazi yake kweli?

“Kocha anayependa kazi yake, lazima akae na wachezaji muda mrefu iwezekanavyo. Nilishangaa kuona kocha msaidizi ndiye aliyekuwa anaongoza mazoezi kabla ya timu kusafiri. Huo ulikuwa uamuzi usio wa kitaalamu kutoka kwa McCarthy, alipaswa kuwepo kuandaa timu.

BEN 02

“Kwa sasa napendekeza FKF watafute kocha mpya. Kwa maoni yangu, kocha wa ndani anaweza kufanya vizuri zaidi. Tunahitaji kumuamini kocha wa ndani na kumpa msaada anaohitaji pamoja na uhuru wa kufanya kazi yake.”

Shimanyula alilalamikia nyota huyo wa zamani wa Manchester United kuhusu kigezo chake cha uteuzi wa wachezaji, akisema kuwa wachezaji wengi wazuri wanaachwa nje ya kikosi.

“Yeye (McCarthy) kila mara huchagua wachezaji kutoka timu chache fulani tu, haendi kutafuta wachezaji zaidi kutoka klabu zingine za Ligi Kuu; uchunguzi wake hautasaidia Kenya.

“Ameshindwa, na hawezi kusaidia Kenya kukua,” alieleza bosi wa Homeboyz na kuongeza:

“Kwa mfano, Homeboyz tuko nafasi ya pili katika Ligi Kuu, lakini hatuna hata mchezaji mmoja Harambee Stars. AFC Leopards wanafanya vizuri sana kwa sasa, lakini hakuna hata mchezaji mmoja kutoka timu hiyo kwenye kikosi cha McCarthy.”

Alikwenda mbali zaidi kuuliza kwa nini mshambuliaji Moses Shumah hayumo kwenye timu. Shumah ndiye alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya FKF msimu uliopita akiwa na mabao 17 kabla ya kuondoka Homeboyz na kujiunga na Power Dynamos ya Ligi Kuu ya Zambia.

Akiwa Dynamos, amekuwa mchezaji muhimu akisaidia timu hiyo kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hadi sasa Shumah amefunga mabao sita kupitia mechi saba za msimu huu katika michuano yote.

“Shumah alienda Zambia, amekuwa akifunga mabao kwa Dynamos, lakini hapati mwito wa timu ya taifa. Ili McCarthy afanikiwe, anahitaji kuunda ushindani ndani ya timu; ana hazina ya wachezaji wazuri nchini kote, na anapaswa kuitumia kuunda ushindani,” alisema Shimanyula na kuongeza:

“Katika kikosi cha sasa, wachezaji wengi wana uhakika wa kuanza mechi. Hii inawafanya baadhi yao kuwa wazembe kwa sababu wanajua hata wakifanya makosa, bado wataanza mechi inayofuata. Lakini ikiwa kutakuwa na ushindani sahihi katika kila nafasi, itawafanya wachezaji wajitume zaidi.

“Kila Mkenya siku hizi anajua ni wachezaji gani wataitwa kila mara McCarthy anapotangaza kikosi, na hii ndiyo inaua timu.”

Kipigo kibaya zaidi katika historia ya Kenya kilitokea mwaka 1961 ilipopoteza 13-2 dhidi ya Ghana katika mechi ya kirafiki ya kuadhimisha Siku ya Jamhuri. Wakati huo, Black Stars walikuwa na kikosi chenye nguvu kilichoongozwa na mshambuliaji hatari Ben Acheampong.