Kenya yaibeba Afrika Olimpiki 2024

Muktasari:

  • Hadi muda huu, Kenya ilikuwa ikishika nafasi ya 17 katika orodha ya timu zenye medali nyingi katika michezo hiyo, ikiwa na medali 11, zikiwa ni nne za dhahabu, mbili za fedha na tano za shaba, ikifuatiwa kwa mbali na Algeria iliyokuwa ya pili kwa nchi za Afrika ikishika nafasi ya 37 ikiwa na medali tatu tu, dhahabu mbili na shaba moja.

WAKATI michezo wa Olimpiki ikitarajiwa kufungwa rasmi leo kuhitimisha siku 19 za msimu wa michezo hiyo inayofanyikia Paris, Ufaransa nchi ya Kenya ndio iliyolibeba bara la Afrika kwa kuongoza katika orodha ya waliobeba medali nyingi, huku China ikiwa vinara kwa sasa ikichuana na Marekani.

Hadi muda huu, Kenya ilikuwa ikishika nafasi ya 17 katika orodha ya timu zenye medali nyingi katika michezo hiyo, ikiwa na medali 11, zikiwa ni nne za dhahabu, mbili za fedha na tano za shaba, ikifuatiwa kwa mbali na Algeria iliyokuwa ya pili kwa nchi za Afrika ikishika nafasi ya 37 ikiwa na medali tatu tu, dhahabu mbili na shaba moja.

Afrika Kusini ndio nchi ya tatu ya Afrika katioka orodha ya wenye medali nyingi, ikiwa ya 42 ikitwaa medali sita zikiwamo moja ya dhahabu,  tatu za fedha na mbili za shaba, ilihali Ethiopia ikiwa ya 45 ikiwa na dhahabu moja, tatu za fedha na kuwa na jumla ya medali nne, huku Misri ikiwa ya 51 na kufunga tano bora kwa Afrika ikiwa na medali tatu ikilingana na nchi za Argentina, Bahrain na Tunisia.

Katika 10 Bora ya orodha ya waliobeba medali nyingi, China ndio kinara ikiwa na medali 90, zikiwamo 39 za dhahabu, fedha 27 na Shaba 24, ikifuatiwa na Marekani yenye  yenye medali t122, zikiwamo 30 za dhahabu, 42 za fedha sawa na zile za shaba, huku Australia ikiwa ya tatu ikizoa medali 50.

Katika medali hizo 50, Australia imevuna 18 za dhahabu, sawa na za fedha na 14 za shaba, ilihali Japan ikiwa na medali 43 ikishika nafasi ya nne ikivuna dhahabu 18, fedha 12 na 13 za shaba, huku wenyeji, imevuna medali 62, zikiwa 16 za dhahabu, 24 za fedha na 22 za shaba.

Nyingine zilizofuta ni Uingereza yenye medali 63 (14-22-27), Uholanzi medali 33 (14-7-12), Korea Kusini medali 30 (13-8-9), huku Ujerumani ikishika nafasi ya tisa ikiwa na medali 31, zikiwamo 12 za dhahabu, 11 za fedha na nane za shaba na nchi ya 10 ni  Italia iliyovuna 39, zikiwamo 11 za dhahabu, 13 fedha na 15 za shaba.