Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kenya kuandaa mashindano ya kikapu wanawake, wanaume

Muktasari:

  • Mashindano hayo mawili muhimu yanaashiria hatua kubwa katika safari ya michezo ya Kenya, yakidhihirisha hadhi yake inayoongezeka katika mpira wa kikapu barani Afrika.

KENYA imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano mawili makubwa barani Afrika ya mpira wa kikapu wanawake (WBLA) na wanaume (Road to Basketball Africa League Elite 16) jijini Nairobi.

Mashindano hayo mawili muhimu yanaashiria hatua kubwa katika safari ya michezo ya Kenya, yakidhihirisha hadhi yake inayoongezeka katika mpira wa kikapu barani Afrika.

Shirikisho la Mpira wa Kikapu Kenya (KBF), lilitangaza habari hizo Alhamisi Oktoba 30, 2025, likieleza kuwa heshima ya kuwa mwenyeji ni tukio la kihistoria katika uongozi wa Kenya unaokuwa kwenye mchezo huo Afrika.

“Mashindano haya mawili mfululizo ni hatua ya kihistoria katika ukuaji wa uongozi na ushawishi wa Kenya ndani ya mpira wa kikapu wa Afrika,” amesema Katibu Mkuu wa KBF, Angela Luchivya.

Mashindano ya WBLA yataanza Novemba 9 hadi 15, 2025, katika Ukumbi wa Nyayo. Yatahusisha klabu bora za wanawake kutoka Kanda ya Tano zikiwemo Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA) na Chuo Kikuu cha Zetech (Kenya), REG na APR (Rwanda), Fox Divers (Tanzania), Gladiators na Hippos (Burundi), pamoja na Magic Stormers (Uganda).

Baada ya kivumbi cha kinadada, macho yataelekezwa kwa Road to BAL Elite 16 mnamo Novemba 18 hadi 23, 2025, katika Ukumbi wa Kasarani. Mashindano hayo ya wanaume yatakutanisha klabu bora kutoka Afrika zikigombea nafasi za kufuzu kushiriki katika BAL ambayo ni ligi kuu ya kitaaluma ya Afrika inayoratibiwa kwa ushirikiano na FIBA na NBA.

Mabingwa wa Kenya, Nairobi City Thunder, watawakilisha taifa. Wanatarajiwa kuonyesha ubabe wao tena baada ya kuvutia mwaka 2024.

Uenyeji wa mashindano hayo mawili unathibitisha hadhi ya Kenya kama ngome ya mpira wa kikapu katika ukanda huu, huku yakionyesha vipaji vya ndani na kuimarisha mshikamano wa michezo Afrika.

KBF imeshukuru Shirikisho la Mpira wa Kikapu barani Afrika (FIBA Africa) na Serikali ya Kenya kwa msaada wao endelevu, na ikatoa wito kwa wadhamini, washirika, na mashabiki kuunga mkono hafla hizi.

“Huu ni wakati wetu wa kuonyesha ulimwengu kwamba Kenya inaweza kuandaa mashindano ya kiwango cha juu,” ameongeza Luchivya.

“Kwa pamoja, tunaweza kuhamasisha kizazi kijacho cha wachezaji na mashabiki, na kusherehekea roho ya umoja wa mpira wa kikapu wa Afrika.”