KCB kukita kambi Meru

KLABU ya KCB inatarajiwa kusafiri hadi kaunti ya Meru wiki ijayo kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na msimu mpya Ligi Kuu Kenya.

Wakiwa huku, KCB inayofundishwa na Zedekiah ‘Zico’ Otieno, itacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Meru Bombers FC na Nanyuki Combine FC.

Kocha Otieno amefurahia kambi hiyo ya mazoezi akisema itasaidia kuimarisha viwango vya utayari wa wachezaji kabla ya kuanza mikikimikiki ya FKFPL.

“Siku zote tunatafuta maeneo ya kuboresha. Safari hii inatupatia fursa kujifunza na kuunganisha zaidi ukizingatia hali ya hewa ya Mlima Kenya inawafaa wavulana kuzoea na pia kuhakikisha wako tayari kwa kazi iliyo mbele yao,” alibainisha Otieno.

KCB imekamilisha usajili wa wachezaji watano wapya zaidi katika dirisha la usajili lililofungwa Septemba 7 mwaka huu ambao ni Hillary Ojiambo kutoka Soy United, Bramwell Kipkorir kutoka Society 43 Nakuru, Edmond Erick kutoka Gogo Boys FC, Kennedy Owino kutoka Wazito FC na Haniff Wesonga moja kwa moja kutoka shule ya upili.

Wanajiunga na kikosi ambacho tayari kilikamisha usajili wa Nicholas Kipkirui, Francis Kairo, Harun Mwale, Kevin Otieno, Danson Chetambe na Byrne Omondi.

Otieno aliweka matumaini na matarajio yake kwa usajili mpya ya kukata kiu kutwaa ubingwa wa kwanza wa FKFPL.