Karia FC kuwakosa nyota wawili

MABEKI wawili wa Karia FC wamepata majeruhi mwishoni mwa wiki jana wakitumikia timu yao kwa katika mechi ya Ligi Kanda ya Kati Zoni E dhidi ya Thika Sharks na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kocha wa Karia FC, Benard Muchai, aliwataja wachezaji hao ni Denis Wanjohi na Daniel Githora ambao walijeruhiwa kisigino na goti.
Alisema nyota hao wawili wa kutegemewa watalazimika kukosa mechi mbili kabla ya kurejea tena uwanjani.
“Baada ya kufanyiwa ukaguzi na daktari imebainika kuwa nyota hao wawili watalazimika kukosa mechi mbili kabla ya kurejea uwanjani,” alisema Muchai.
Karia FC inakamata nafasi ya tisa ikiwa imejikusanyia pointi 15 katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Timu hiyo imeshuka dimbani mara 13 ikifanikiwa kushinda mechi tano na kupoteza michezo nane huku wakibakisha mechi dhidi ya Theta KTDA FC na Infinity FC kabla ya kumaliza mzunguko wa kwanza.
“Ningetamani kukamilisha mkondo wa kwanza wa ligi nikiwa nafasi nzuri ili kujitayarisha vyema kwa mkondo wa pili,” alisema kocha Muchai.