KALEKWA: WANAHABARI WAPO NDANI NDANI KWENYE MATCH-FIXING

MULIKI wa klabu ya Sofapaka, Elly Kalekwa sasa kaowaongeza wanahabari kwenye sakata la Match Fixing, ishu inayozidi kuibua mdahalo mkubwa nchini.
Akizungumza baada ya lile sakata la Zoo Kericho wiki iliyopita iliyowapelekea kushushwa daraja na FIFA hadi divisheni ya tatu Division One League, kwa tuhuma za upangaji matokeo mechi, Kalekwa kadai janga hilo limekita mizizi.
Kulingana naye hata wanahabari sasa wako game kinoma kwenye masakata haya ya upangaji mechi
Kalekwa anadai kuwa pia nao baadhi ya viongozi wa klabu wanajihusisha na visa hivi vya match-fixing kwa sababu ya tamaa za hela.
Lakini anachosema kinamuumiza zaidi ni kuowana wanahabari wa michezo nao wakiwa wamejiongeza kwenye masakata haya ya upangaji matokeo mechi.
“Suala la match-fixing katika taifa hili sio siri tena. Lipo wazi. Janga hili limeota mizizi na hofu yangu sasa ni kuwa siku moja ligi zetu zitakuja kupigwa marufuku.” Katanguliza Kalekwa.
Mfanyibiashara huyo anasema hofu hiyo imempelekea yeye kuwakusanya baadhi ya wadau wa soka nchini na kufanya kikao na FKF kujadili kuhusu namna ya kuangamiza janga hili.
“Kuna mengi yasiyofahamika kuhusu  ishu hii ya upangaji matokeo mechi. Wakati watu wengi wanadhani ni wachezaji tu ndio wahusika wakuu, kunao wengine. Hapa nawasemea baadhi ya viongozi wa klabu lakini kinachonisikitisha hata zaidi ni kwamba baadhi ya waaandishi wa michezo wapo katikati ya masakata haya. Wapo ndani ndani kabisa.” Kalekwa kasisitiza.
Sio siri kuwa baadhi ya wanahabari wa michezo nchini pia ni mawakala wa baadhi ya wachezaji wanaosakata soka la kulipwa nje na ndani ya nchi.
Kalekwa anasema jambo hili linamuumiza sana hasa akizingatia namna alivyowekeza mamilioni ya pesa kwenye uimarishaji wa Sofapaka iliyopanda ligi kuu 2009.