K’Ogalo, Rangers jino kwa jino

RAUNDI ya tatu Ligi Kuu Kenya imemalizika ikishuhudia mabadiliko kileleni ila huko mkiani bado hakuna jipya.

Wikendi imekuwa tamu kwa Posta Rangers na mabingwa watetezi Gor Mahia waliyomuondoa Murang’a Seal usukani mwa FKFPL.

Wageni hao wa ligi, walianza msimu kwa moto wakiwafinya wageni wenzao Shabana na washindi wa Mozzart Bet Cup, Kakamega Homeboyz, lakini mwishoni mwa wiki wakakumbushwa kwenye ligi mambo ni matatu; ushinde, utoe sare au upoteza.

Kwa bahati mbaya, Murang’a Seal walipoteza kwa FC Talanta wakiruhusu bao la ‘usiku’ lililofungwa na Alex Juma hivyo kushushwa hadi nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi zao sita.

Nao Rangers ambayo msimu uliyopita walimaliza nafasi ya 12, wamekuwa na mwanzo mzuri wakiwa hawajapoteza mchezo na wapo kileleni na pointi saba sawa na Gor Mahia ila wamewazidi mabingwa hao watetezi kwa ubora wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mchezaji wa zamani wa AFC Leopards, Peter Thiong’o, aliweka kambani mabao mawili katika ushindi wa 3-1 waliyopata Rangers dhidi ya Sofapaka waliyo nafasi ya pili kutoka mwisho na bado wanaendelea kusaka ushindi wao wa kwanza.

Kama ilivyokuwa kwa Thiong’o, ndivyo ilivyokuwa kwa straika wa K’Ogalo, Benson Omala ambaye amepania Kiatu cha Dhahabu msimu huu, alipofunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Nairobi City Stars.

Ni ushindi uliyokuja na gharama yake kwani inadaiwa wezi walijipenyeze kwenye vyumba vya kubadilisha nguo Uwanja wa Kasarani na kuondoka na pesa pamoja na simu za wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi.

Huko mkiani, mambo bado ni magumu kwa Ulinzi Stars wakipoteza mchezo wao wa tatu mfululizo walipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Bandari FC ambao wapo nafasi ya tatu kwa pointi sita.

Presha pia ipo kwa magalacticos, Kenya Police FC, wakiendelea kusaka ushindi wao wa kwanza baada ya mwishoni mwa wiki kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Shabana FC.

Timu zingine ambazo hazijaonja ladha ya ushindi hadi sasa msimu huu ni Sofapaka, City Stars, AFC Leopards, Shabana na Muhoroni Youth.