Ingwe yabanwa ugenini, Sofapaka ikilala nyumbani
Muktasari:
- Dakika 10 kabla ya mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Dondora, jijini Nairobi ziliikatilia Ingwe baada ya wenyeji kuchomoa bao.
MABINGWA wa zamani wa Kenya, AFC Leopards ikicheza ugenini imenyang'anywa tonge mdomoni jioni na Posta Rangers baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mechi ya Ligi Kuu (KPL).
Dakika 10 kabla ya mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Dondora, jijini Nairobi ziliikatilia Ingwe baada ya wenyeji kuchomoa bao.
AFC ilianza kuandika bao la kwanza dakika 23 kupitia kwa Kelly Madada kabla ya wenyeji kuchomoa dakika kumi baadae baada ya Jackson Dwang kukwamisha wavuni na hadi mapumziko matokeo yalikuwa bao 1-1.
Ingwe ilirudi kipindi cha pili kwa kasi na kuandika bao la pili dakika ya 49 kupitia Ssenyonjo Samuel.
Hata hivyo, dakika ya 80 Posta Rangers ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Eliud Lokowam na kufanya matokeo kuwa 2-2 na timu kugawana pointi ambapo Posta ilirejea kileleni kwa kufikisha saba baada ya mechi tatu ikiishusha Shabana yenye pointi sita ikicheza mechi mbili kama AFC iliyo na pointi mbili kwa sasa.
Katika mechi nyingine wenyeji Sofapaka ilijikuta ikilala nyumbani kwa kufungwa bao 1-0 na Kakamega Homeboyz.
Bao hilo la washindi liliwekwa kimiani na Josphat Lopaga dakika ya tatu tu ya mechi hiyo na kuifanya Kakamega ipande kutoka nafasi yab12 hadi ya tano katika msimamo wa Ligi hiyo yenye timu 18 kwa kufikisha pointi nne baada ya mechi tatu, huku Sofapaka ilisalia nafasi ya 16 ikiwa na pointi moja kupitia mechi mbili ilizocheza hadi sasa.