Hii ndiyo Bandari FC itakayocheza dhidi ya Yanga
Muktasari:
- Katika tamasha hilo, Yanga itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Bandari FC ya Kenya, mechi ambayo itatumika kama kipimo cha wachezaji wapya waliotua Jangwani kwa ajili ya kuongeza nguvu katika maeneo tofauti, kuanzia nyuma hadi kwenye safu ya ushambuliaji.
LEO ni ile siku ambayo mashabiki wa Yanga maarufu kama Wananchi, walikuwa wakiisubiri kwa hamu. Ni kilele cha tamasha lao kubwa la kila mwaka ambalo huashiria kuanza rasmi kwa msimu mpya.
Katika tamasha hilo, Yanga itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Bandari FC ya Kenya, mechi ambayo itatumika kama kipimo cha wachezaji wapya waliotua Jangwani kwa ajili ya kuongeza nguvu katika maeneo tofauti, kuanzia nyuma hadi kwenye safu ya ushambuliaji.
Miongoni mwa wachezaji ambao wanasubiriwa kwa hamu kutazamwa ni pamoja Celestin Ecua kutoka Zoman FC na Mohamed Doumbia kutoka Majestic, Balla Moussa Conte (CS Sfaxien, Tunisia), Offen Chikola (Tabora United), Lassine Kouma (Stade Malien), Andy Boyeli (Sekhukhune) na Mohammed Hussein (Simba).
Makala haya yanakuchambulia kuhusu timu hiyo ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Kenya ikiwa na pointi 44, haikushinda katika mechi zake tano za mwisho.
Bandari ilitoa sare nne katika mechi hizo tano dhidi ya Posta Rangers (1-1), Mathare United (0-0), Leopards (0-0), Mara Sugar na ikachapwa bao 1-0 dhidi ya Polisi iliyotwaa ubingwa wa msimu uliopita.
CHIMBUKO LAKE
Bandari maskani yake ni mjini Mombasa, timu hiyo inacheza mechi zake za nyumbani kwenye viwanja viwili, Mbaraki na Mombasa County.
Historia ya Bandari ni ndefu. Ilianza mwaka 1960 kama LASCO, kisha ikawa Cargo kabla ya kuungana na kikosi cha Kenya Ports Authority (KPA) mwaka 1985 kuunda Bandari ya sasa.
Baada ya kupanda na kushuka daraja mara kadhaa, ilirejea kwa kishindo Ligi Kuu, ikawa mshindi wa pili mwaka 2017 na 2018 na ilinyakua taji la SportPesa Super Cup 2018, jambo lililowapa nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hiyo ilikabiliana na Al Ahly Shendi na kutoka suluhu nyumbani kabla ya sare ya 1-1 ugenini Shendi, Sudan na hivyo kuifungashia virago timu hiyo ya Sudan. Katika raundi ya pili ilikabiliana na US Ben Guardane ya Tunisia na iliwaondoa kwa njia ile ile.
Timu hiyo ilifutwa mwaka 1999, lakini ilirejeshwa tena mwaka 2004 na haraka ikapanda kutoka ligi za chini hadi Ligi Kuu.
Klabu hiyo ilifika fainali ya Kombe la Kenya mwaka 1986, lakini ilishindwa na Gor Mahia ambayo ilishiriki Kombe la washindi Afrika mwaka uliofuata na hatimaye kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
KIKOSI CHAO
Kwa sasa, kikosi cha Bandari kina wastani wa umri wa miaka 26.3, wakiwa na wachezaji wa ndani na wachache wa kigeni (asilimia 25).
Baadhi ya nyota muhimu wanaotarajiwa kuibeba timu hii ni pamoja na Joseph Okoth, Andrew Juma, Edward Satulo.
Wengine ni Siraj Mohammed, Michael Sunday Apudo, Jackson Dwang ambaye ni kiungo wa kati kutoka Sudan Kusini, William Wadri, mshambuliaji hatari kutoka Uganda mwenye umri wa miaka 29.
Hawa ndio wachezaji ambao Yanga italazimika kuwaheshimu, kwani wana uzoefu mkubwa kwenye ligi ya Kenya na mashindano ya kimataifa.
KOCHA WAO
Kocha wa Bandari ni Ken Odhiambo. Aliteuliwa rasmi kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Julai 2024, akichukua nafasi ya John Baraza.
Odhiambo, ambaye pia ni msaidizi wa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Benni McCarthy, alirudi Bandari kwa mara ya tatu, akiwa na lengo la kurejesha mafanikio ya klabu hiyo.
Katika kipindi chake cha hivi karibuni, Odhiambo alieleza atatumia michezo ya mwisho ya msimu wa 2024–2025 ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kama maandalizi kwa msimu ujao, akijaribu wachezaji katika nafasi tofauti.
Kwa sasa, Odhiambo anasaidiwa na John Baraza, ambaye alikalia kiti cha ukocha baada ya Twahir Muhiddin kuondolewa.