Gor Mahia yapindua meza, sasa uso kwa uso na Al Ahly

Muktasari:

  • K'Ogalo iliwanyong'onyesha mashabiki wa timu hiyo wiki iliyopita ilipochapwa bao 1-0 mjini Juba, Sudan Kusini, lakini mchana huu ilishuka kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, jijini Nairobi na kuwapa furaha kwa kupata ushindi huo wa kishindo na kusonga mbele.

MABINGWA wa soka wa Kenya, Gor Mahia wamefanya kile ambacho mashabiki walikitarajia baada ya kuifumua Al Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa mabao 5-1 na kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa itakutana na watetezi wa taji hilo, Al Ahly ya Misri.

K'Ogalo iliwanyong'onyesha mashabiki wa timu hiyo wiki iliyopita ilipochapwa bao 1-0 mjini Juba, Sudan Kusini, lakini mchana huu ilishuka kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, jijini Nairobi na kuwapa furaha kwa kupata ushindi huo wa kishindo na kusonga mbele.

Wageni waliwashtua K'Ogalo kwa kufunga bao la mapema la dakika ya nane kupitia Samuel Akinbinu kabla ya Chris Ochieng kusawazisha dakika ya 13.

Wakati Al Merrikh ikijiuliza cha kufanya, ikapigwa bao la pili lililowekwa kimiani dakika ya 22 na Alpha Onyango na daklika 10 kabla ya mapumziko, Alphonce Amija akafunga bao la tatu.

Kipindi cha pili Wasudan walikomaa na kupunguza kasi ya wenyeji, hata hivyo dakika tisa za mwishoni wakashindwa kuendelea kushikilia bomba na kujikuta wakiruhusu mabao mawili yaliyofungwa dakika ya 81 na 90 kupitia kwa Rooney Onyango.

Matokeo hayo yanaifanya sasa Gor Mahia kusonga mbele raundi ya pili kwa kukutana na mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri ikianzia nyumbani Septemba 14 kabla ya wiki moja baadae kurudiana nao jijini Cairo ili kusaka nafasi ya kutinga makundi.