Gor Mahia yaaibishwa nyumbani, yapigwa 4-1
Muktasari:
- K'Ogalo ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia mshambuliaji Mghana George Amonoo dakika ya tano ya pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi.
MABINGWA wa zamani wa Kenya, Gor Mahia wametiwa aibu nyumbani jioni hii baada ya kufumuliwa kwa mabao 4-1 na A.P.S Bomet katika mechi ya Ligi Kuu (KPL).
K'Ogalo ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia mshambuliaji Mghana George Amonoo dakika ya tano ya pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi.
Hata hivyo, wageni walipambana na kupata penalti dakika 39 iliyowekwa wavuni na kiungo Hansel Ochieng na kuisawazishia A.P.S Bomet.
Dakika tatu baada Ochieng akaiongezea A.P.S bao la pili na kufanya iende mapumziko ikiwa mbele ya K'Ogalo kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili, timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji, lakini ni A.P.S iliyonufaika kwa kufunga mabao mengine wawili dakika za 77 na 87 na kupata ushindi wa pili katika ligi hiyo na kutoka mkiani mwa msimamo kwa kufikisha pointi nane ikiiachia msala Kariobang Sharks iliyorudia mkiani ikiwa na alama saba tu kwa michezo tisa.
Ochieng alifunga bao la tatu akikamilisha hat trick yake jioni hii mbele ya Gor na Rodgers Kipkemoi alikamilisha hesabu kwa kupigilia msumari wa mwisho wa jeneza na K'Ogalo dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho.
Hicho ni kipigo cha pili kwa K'Ogalo msimu huu katika Ligi Kuu kupitia mechi tisa, japo imeendelea kusalia kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 19.