Gor Mahia, Tusker kitaumana

MAZE! Kuna jitu linakufa leo Jumatano Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi pale watakapokutana miamba mwili ambayo kwa miaka 11 sasa wamekuwa wakibadilishana ubingwa wa Ligi Kuu Kenya.

Mabingwa wa kihistoria, Gor Mahia, watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Tusker FC katika muendelezo wa ngarambe za FKFPL ambapo leo Jumatano zinapigwa mechi saba na mbili Alhamisi katika viwanja tofauti.

K’Ogalo watashuka dimbani wakijivunia ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mwisho dhidi ya Nairobi City Stars.

Kwa mara nyingine tena, macho yatamulikwa kwa straika Benson Omala ambaye alifunga bao la pekee dhidi ya City Stars na kumfanya kufikisha mabao 11 hadi sasa msimu huu akiendelea kukimbiza Kiatu cha Dhahabu.

Gor wapo katika fomu nzuri wakiwa hawajapoteza mchezo katika mechi zake tano za mwisho wakishinda tatu na kutoa sare mbili na wanaikabili Tusker FC inayochechemea licha bado wamo kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Wanamvinyo hao wamelazimishwa sare tatu katika michezo yao tano ya mwisho huku wakishinda moja na kupoteza mchezo moja.

Tusker FC nusura wapoteza mchezo wao wa mwishoni mwa wiki iliyopita lakini David Majak alitumia vyema assist ya kipa Patrick Matasi kuisawazishia timu yake dakika ya 77 baada ya Tyson Otieno kuitanguliza Kariobangi Sharks dakika ya 49.

Mechi ya kesho inayotazamiwa kuwa kali na ya kusisimua itashuhudia makocha wawili noma lakini kuna gepu kubwa la umri, miaka 21, ambapo mkufunzi wa Tusker FC, Robert ‘Simba’ aliyezaliwa Aprili 6, 1964 ana miaka 58 wakati Jonathan McKinstry wa Gor Mahia aliyezaliwa Julai 16, 1985 ana umri wa miaka 37.

Ni mbinu za kocha mkongwe dhidi ya kocha kinda zitakazoamua mtangange wa kesho japo jambo lililowazi ni kuwa wote ni wazoefu katika taaluma ya ukocha.

Ushindi kwa K’Ogalo utawafikisha pointi 30 hivyo kuwaacha Tusker FC kwa pointi tano lakini kama vijana wa Matano wataibuka na ushindi, watawazidi Gor Mahia kwa pointi moja.

Katika mechi nyingine itakayopigwa kesho, vinara wa FKFPL, Nzoia Sugar, wanasaka kuendelea kujikita kileleni hususan baada ya sare yao tasa dhidi ya AFC Leopards watakapokuwa wageni wa Kariobangi Sharks.

Kenya Police FC wanaokimbiza ubingwa kimya kimya wanashuka dimbani kesho kuikabili City Stars huku Sofapaka ambayo msimu wao umekuwa ya kusuasua wanaivaa KCB ambayo haijapoteza mchezo wowote mwaka huu.  

Patashika tamu nyingine kesho ni kati ya Mathare United dhidi ya Vihiga Bullets zote zikiwa mkiani baada ya kila moja kujikusanyia pointe nne.


RATIBA KAMILI

Leo Jumatano

City Stars v Police FC

Gor v Tusker

Mathare v Vihiga Bullets

Ulinzi v Bidco

Bandari v Homeboyz

Sharks v Nzoia

Sofapaka v KCB


Kesho Alhamisi

Rangers v Wazito

Talanta v Leopards