Gor Mahia, Nzoia freshi barida
BUDA! Kuna mtu ataumia Gor Mahi na Nzoia Sugar zitakapokutana kesho Jumatano mzunguko wa pili Ligi Kuu Kenya (FKFPL) uking’oa nanga.
Mechi hii ya kukata na shoka itapigwa katika Uwanja wa Sudi uliyopo Kanduyi, Kaunti ya Bungomo na unatarajiwa kuvuta mashabiki wengi kutoka eneo la Magharibi na kaunti zilizopo jirani.
Pointi nne tu ndizo zinazozitenganisha timu hizi mbili ambapo K’Ogalo inayonolewa na Jonathan McKinstry ipo kileleni na pointi zake 37 wakati vijana wa Salim Babu, Nzoia Sugar, wanawapumulia kwa kujikusanyia pointi 33.
Nzoia Sugar ambao ndiyo wenyeji wa pambano hilo, wataingia dimbani wakiwa freshi baada ya mapumziko ya takribani siku 10 wakati kwa Gor Mahia, ni hakuna kulala kutokana na kucheza mechi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Naam! K’Ogalo walikuwa uwanjani kuwajibika katika mchezo wa Kombe la FKF ambao wao ni mabingwa watetezi na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kibera Soccer lililofungwa na Lloyd Khavuchi.
Hata hivyo ilikua mechi ambayo kocha McKinstry alitumia zaidi wachezaji wa kikosi cha pili akipumzisha mastaa yake kwa ajili ya mechi ya kesho ukizingatia Nzoia Sugar hawakua na mechi yoyote wikendi iliyopita kwasababu hawakudhibitisha ushiriki wao wa Kombe la FKF inayojivunia udhamini wa kampuni ya kubeti ya Mozzart Bet.
Timu hizi mbili hazikuvuna ushindi katika michezo yao ya mwisho ya FKFPL ambapo Gor Mahia walichezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mathare United huku Nzoia Sugar wakilazimishwa sare tasa na FC Talanta.
Utamu wa mechi hii unatokana na Gor kushinda ngarambe ya mzunguko wa kwanza bao 1-0 lililofungwa na Benson Omala hivyo watataka kuendeleza ubabe wao na kuongeza wigo wa pointi dhidi ya Nzoia Sugar ambao kwa upande wao wamepania kulipiza kisasi na kupunguza pengo la pointi.
Mechi nyingine kesho Jumatano katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi ni kati ya onform AFC Leopards dhidi ya Wazito FC ambayo iko katika hatari ya kushuka daraja.
Leopards chini ya ukufunzi wa Patrick Aussems imekua na matokeo mazuri ikishinda mechi sita kati ya tisa za hivi karibuni ikiweka ‘cleansheet’ nane mfululizo.
Mara ya mwisho Ingwe kufungwa ilikua Januari 14 mwaka huu na walifungwa na Wazito FC mabao 2-1 mechi ambayo Aussems alimuelekezea kidole cha lawama refa ya ngarambe hiyo.
Hivyo basi, Leopards watakuwa wanashuka dimbani wakiwa na kazi mbili; kulipiza kisasi dhidi ya Wazito FC na kushinda kuendelea kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa FKFPL msimu huu.
Nako kwa Wazito FC ambayo imepata kocha mpya, Charles Odero baada ya Jeffers Odongo kubwaga manyanga, inasaka ushindi wake wa tatu msimu huu ili kuanza kampeni ya kuondoka mkiani.
RATIBA FKFPL
Kesho Jumatano
Sofapaka v Mathare
Bidco v City Stars
Vihiga v Rangers
KCB v Talanta
Leopards v Wazito
Nzoia v Gor Mahia
Ulinzi Stars v Homeboyz
Police v Sharks