Ghost Mulee amuonya Abdallah

Ghost Mulee amuonya Abdallah

Summary

  • KOCHA Jacob ‘Ghost’ Mulee kamtaka staa mpya wa Harambee Stars, Hassan Abdallah asichochwe na sifa anazopata baada ya kuendelea kung’aa na timu ya taifa.

KOCHA Jacob ‘Ghost’ Mulee kamtaka staa mpya wa Harambee Stars, Hassan Abdallah asichochwe na sifa anazopata baada ya kuendelea kung’aa na timu ya taifa.

Wing’a huyo wa Bandari FC kaendelea kuthibitisha ni kwa nini itakuwa vigumu sana kumnyima kikosini.

Katika mechi nne za mwisho za Stars mchango wake umekuwa mkubwa mno kwa timu hiyo ya taifa na dhidi ya South Sudan mechi ya kirafiki mwezi uliopita, alipoteza fursa mbili za wazi za kupachika bao lakini akahusika kwenye utengenezaji wa bao la ushindi lilipopachikwa na Elvis Rupia, huku akipachika moja dhidi ya Tanzania kwenye ushindi wa mabao 2-1 akitokea benchi.

Pia alifunga dhidi ya Misri mechi ya kufuzu Afcon 2021,kabla ya Stars kusafiri hadi jijini Lome, kumalizana na Togo na alipachika bao moja kwenye ushindi wao wa 2-1.

Katika mechi nne za mwisho za Stars, wing’a huyo kapachika mabao manne na kuendelea kupokea sifa kibao kutokana na kiwango chake kizuri kutoka kwa mashabiki, makocha na wachanganuzi wa soka nchini.

Kocha Ghost mwenyewe kakiri wazi wazi kupagawishwa na kiwango cha wing’a huyo wa kulia kubwa zaidi linalomvutia ni jinsi anavyojiamini licha ya kuwa mgeni sana kwenye timu ya taifa.

Lakini pamoja na sifa zote hizo, jambo hilo sasa linampa hofu kidogo kocha Ghost ambaye kamshauri Abdallah kuwa makini na kuhakikisha halewi sifa hizi anazopata kwani zinaweza kuathiri kiwango chake.