FKF-PL YARUDI NA UBAYA, MECHI KUCHEZWA KILA SIKU

Friday May 07 2021
FKF PIC
By Thomas Matiko

KLABU zinazoshiriki ligi kuu ya FKF-PL msimu huu zitalazimika kucheza mechi mbili mbili kila wiki, ligi hiyo itakaporejelewa Mei 12, 2021.
Msimu huu wa 2020/21 ulisitishwa Machi 26, kufuatia amri ya Rais Uhuru Kenyatta kusitisha michezo yote nchini kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya Covid-19.
Baada ya kuiondoa lockdown hiyo kwenye sherehe za Leba dei Jumamosi iliyopita, Shirikisho la soka nchini FKF sasa limeachia ratiba mpya ya mechi zilizosalia.
Hadi kufikia kusitishwa kwa ligi hiyo, ni mechi 15 ndizo zilizokuwa zimechezwa. Bado mzunguko wa kwanza wa ligi msimu huu haukuwa umekamilika ukiwa umesalia na mechi nne.
Kulingana na ratiba hiyo mpya, Wazito FC watuchuana na mabingwa watetezi Gor Mahia katika uwanja wa Kasarani., Nairobi.
Siku hiyo tu kutakuwa na ngoma nyingine nzito kati ya AFC Leopards na Mathare United utakaochezewa uwanja uo huo.
Mechi za raundi ya 17 zitachezwa kati ya Mei 14 hadi Mei 16 kabla ya Gor Mahia na Mathare kuchezea mechi yao iliyoratibiwa upya dhidi ya Sofapaka na KCB katika usanjari huo.
Kuanzia mechi za raundi 18, ngoma zitapigwa kila siku hadi Mei 29. Baada ya hapo ligi itachukua mapumziko ya wiki mbili ili kupisha michuano ya kimataifa ambapo Harambee Stars watakuwa na kibarua dhidi ya Uganda kwenye mechi ya kwanza ya kufuzu kushiriki kombe la dunia 2022 kule Qatar.
Mechi hiyo itachezwa Juni 6, katika uwanja wa Nyayo na kisha timu hiyo ya taifa iburuke hadi Kigali, kufinyana na Rwanda hapo Juni 13.
Kulingana na FKF, utaratibu huu ni kuhakikisha kwamba soka la Kenya linaweza kuendana na kalenda ya CAF na ile ya FIFA.

Advertisement