Fainali ya rekodi, heshima CHAN 2024
Muktasari:
- Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu, Madagascar inatafuta historia ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza, huku Morocco maarufu kama Atlas Lions ikitaka kuendeleza ubabe wa kuchukua ubingwa huo mara ya tatu.
FAINALI ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN 2024), inapigwa leo kwenye Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi, Kenya, ambapo Madagascar itakuwa na kibarua cha kupambana dhidi ya Morocco kuanzia saa 12:00 jioni.
Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu, Madagascar inatafuta historia ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza, huku Morocco maarufu kama Atlas Lions ikitaka kuendeleza ubabe wa kuchukua ubingwa huo mara ya tatu.
Sherehe ya kufunga mashindano imeanza tangu saa 8 mchana na kuhudhuriwa na viongozi mashuhuri akiwemo, Rais William Ruto wa Kenya na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, pamoja na wasanii mbalimbali wanaotoa burudani.
Kwa mujibu wa CAF, wasanii walioteuliwa ni wale wanaowakilisha nchi zote tatu za Tanzania, Kenya na Uganda ambao ndio walioandaa michuano hiyo, huku burudani ya muziki ikizingatia zaidi utamaduni wa mila za mataifa hayo yote matatu.
Wasanii wanaotumbuiza katika fainali hiyo ni Zuhura Othman maarufu 'Zuchu' kutoka Tanzania, muandaaji na mwandishi wa nyimbo kutokea Kenya, Savara Mudigi anayejulikana zaidi kwa jina la Savara na mwimbaji maarufu wa Uganda, Eddy Kenzo.
Morocco ambao ni mabingwa wa CHAN mara mbili (2018 na 2020), inataka kuthibitisha ubabe katika michuano ya mwaka huu, huku Madagascar inayoshiriki mara ya pili inapambana kuandika rekodi mpya kwa mara ya kwanza.
Madagascar ilianza michuano ya CHAN 2024 ikimaliza nafasi ya pili kundi B na pointi saba sawa na Mauritania iliyokuwa ya tatu ila zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, nyuma ya vinara na wenyeji, Tanzania iliyomaliza na pointi 10.
Katika hatua ya robo fainali kikosi hicho kikaitoa wenyeji, Kenya kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya sare ya kufungana bao 1-1, dakika 120, kisha nusu fainali ikaendeleza maajabu kufuatia kuichapa Sudan bao 1-0 na kutinga fainali kibabe.
Kwa upande wa Morocco ilianza michuano hiyo ikimaliza nafasi ya pili kundi A na pointi tisa, baada ya kushinda mechi tatu na kupoteza moja tu kati ya nne iliyocheza, nyuma ya wenyeji Kenya iliyoibuka kinara kufuatia kukusanya pointi 10.
Katika hatua ya robo fainali, Morocco iliiduwaza wenyeji, Tanzania kwa kuichapa bao 1-0, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kisha nusu fainali ikaichapa mabingwa watetezi Senegal kwa penalti 5-3, baada ya sare ya bao 1-1.
Akizungumzia fainali hiyo, Kocha wa Madagascar, Romuald Rakotondrabe (60), amesema ushindi wa leo utakuwa ni tumaini kwa wananchi wa nchi hiyo kutokana na changamoto mbalimbali wanazopitia sasa, ikiwemo hali ngumu ya kiuchumi.
"Tunaiheshimu Morocco, lakini haina maana Madagascar hatustahili kushinda. Tuko katika fainali kwa ajili ya kushindana licha ya kuwakosa wachezaji wetu watatu akiwemo mshambuliaji Fenohasina Gilles Razafimaro mwenye kadi nyekundu," amesema.
Kocha wa Morocco, Tarik Sektioui amesema kushinda michuano ya CHAN kutampa heshima ya kukuza na kuendeleza soka la nchi hiyo, lakini pia kwake binafsi itakuwa ni mafanikio makubwa kwa sababu itamuongeza wasifu (CV) maishani.
"Katika michuano yoyote ile huwa hatudharau mpinzani tunayekutana naye, safari yetu haikuwa rahisi kwa sababu tumesafiri nchi zote tatu za Kenya, Uganda na Tanzania, jambo ambalo limetupa motisha zaidi kwetu ya kushinda taji," amesema Tarik.
Michuano hiyo iliyoanza Agosti 2, 2025 na kuhitimishwa leo Agosti 30, 2025 ikishirikisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda, bingwa atachukua kiasi cha Dola 3.5milioni, huku wa pili akichukua Dola 1.2milioni.