Mkenya aingia rada za Singida Black Stars
Muktasari:
- Nyota huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili, amebakisha miezi sita baada ya msimu huu wa 2025-2026 kuisha, ingawa kwa sasa mabosi wa Pamba wameanza mazungumzo ya kuongeza mwingine, japo inakabiliwa na upinzani kutoka Singida Black Stars.
WAKATI uongozi wa Pamba Jiji ukiwa katika mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mkenya Mathew Momanyi Tegisi baada ya kuridhishwa na kiwango chake, Singida Black Stars imeingilia kati na kuhitaji saini yake.
Nyota huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili, amebakisha miezi sita baada ya msimu huu wa 2025-2026 kuisha, ingawa kwa sasa mabosi wa Pamba wameanza mazungumzo ya kuongeza mwingine, japo inakabiliwa na upinzani kutoka Singida Black Stars.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji (CEO), Peter Juma Lehhet amesema uongozi unafanya jitihada za kumuongezea mkataba mpya nyota huyo na tayari taratibu za majadiliano kati ya pande zote mbili zimeanza kufanyika.
“Kuna wachezaji tunaendelea na mazungumzo nao kwa ajili ya kuongeza mkataba mpya na tutakapofikia muafaka tutaweka wazi juu ya hilo, kwa sasa malengo yetu ni kuhakikisha tunamaliza msimu vizuri kwa mechi zetu zilizobakia,” amesema Lehhet.
Licha ya kauli ya Lehhet ila Mwanaspoti linatambua uongozi wa Singida umevutiwa na kiwango cha mshambuliaji huyo raia wa Kenya, ambapo inaangalia uwezekano wa kumpata baada ya msimu huu kuisha, jambo linaloongeza ushindani kati ya timu hizo.
Momanyi aliyetokea Shabana ya Kenya, alijiunga na Pamba dirisha dogo la Januari 2025 na hadi mwisho wa msimu wa 2024-2025, alifunga mabao saba ya Ligi Kuu, akiwa ndiye aliyeongoza katika kikosi hicho cha ‘TP Lindanda’ au ‘Wana Kawekamo’.
Nyota huyo aliendeleza alipoishia akiwa na Shabana FC, kwa sababu kabla ya kujiunga na Pamba alikuwa pia amefunga mabao matano kwao Kenya, nyuma ya mshambuliaji mwingine wa kikosi hicho, Brian Michira aliyekuwa anaongoza kwa kufunga saba.
Msimu huu wa 2025-2026, tayari nyota huyo amefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara akiwa ndiye anayeongoza ndani ya kikosi hicho pia, huku mabao yake ya mwisho kufunga ni ya kichapo cha Pamba cha 3-2, dhidi ya Tanzania Prisons, Mei 26, 2026.