Danadana FKFPL zinaendelea

KWA mara nyingine tena Kamati ya Mpito ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), hapo jana ilitoa taarifa kuhairisha kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Kenya 2022/23 huku zikiwa zimesalia siku 14 kabla muda wao haujakwisha.

FKFPL ilikua ianze leo hii ikiwa ni baada ya kuhairishwa mara tatu na kamati hiyo iliyoundwa na Waziri wa Michezo anayeondoka Balozi Amina Mohamed na haijataja tarehe mpya.

“Tunaomba kuwajulisha ligi ya msimu 2022/23 ambayo ilitarajiwa kuanza Oktoba 1 imehairishwa. Tarehe ya kuanza ligi hiyo itatangazwa hapo baadaye,” ilisomeka ujumbe wa kamati ya mpito.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa maamuzi ya kuhairisha kuanza msimu mpya imetokana na maombi ya klabu hadi pale wadau wataamua njia muafaka.

Rais wa FKF aliyepigwa stop na Serikali, Nick Mwendwa, alidokeza msimu mpya wa FKFPL utaanza mwishoni mwa mwezi huu.

Wakati huo huo kamati hiyo imetoa ripoti ya maendeleo inayoelezea mapendekezo 12 ya kuzingatiwa na kupitishwa baada ya kumalizika kwa muda wao.