Dabi ya Mashemeji yaahirishwa kutokana na ukosefu wa uwanja
Muktasari:
- Dabi hiyo imeahirishwa baada ya Gor Mahia, iliyopaswa kuwa mwenyeji, kuiandikia Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ikieleza kushindwa kupata uwanja unaofaa kwa mechi hiyo maarufu na yenye changamoto kubwa za kiusalama.
Mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Kenya kati ya mahasimu wakuu, Gor Mahia na AFC Leopards, iliyotarajiwa kuchezwa Jumamosi Novemba 29, 2025, imeahirishwa kutokana na kukosekana kwa uwanja.
Dabi hiyo imeahirishwa baada ya Gor Mahia, iliyopaswa kuwa mwenyeji, kuiandikia Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ikieleza kushindwa kupata uwanja unaofaa kwa mechi hiyo maarufu na yenye changamoto kubwa za kiusalama.
“Kutokana na changamoto hii, tunaomba kwa heshima kwamba mechi hii iahirishwe hadi tarehe nyingine mtakayotoa taarifa baadaye,” amesema Katibu Mkuu wa Gor Mahia, Nicanor Arum, katika barua yake kwa Meneja wa Ligi na Mashindano wa FKF, Frank Ogolla.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote unaoweza kujitokeza na tunawahakikishia dhamira yetu ya kuhakikisha mechi hii inachezwa kwa utulivu mara tarehe mpya itakapothibitishwa,” ameongeza Arum.
“Tukio hili haliwezi kufanyika bila uwanja, hivyo dabi imeahirishwa,” amesema Mkuu wa Mawasiliano, Vyombo vya Habari na Uhusiano wa Umma wa FKF, Jeff Kinyanjui.
Awali, mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumapili Novemba 30, 2025 kwenye Uwanja wa Moi, Kasarani.
Hata hivyo, baadaye yalifanyika mabadiliko na kupelekwa Uwanja wa Nyayo, siku ya Jumamosi Novemba 29, 2025 ili kutoa nafasi kwa Nairobi United kuikaribisha AS Maniema Union ya DR Congo kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Jumapili.
Kuihamishia Uwanja wa Nyayo, kunainyima mechi hiyo kuchezwa Jumamosi kwani siku hiyo Nairobi United na AS Maniema Union zinatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kupambana Jumapili.
Imebainika pia Gor Mahia haiwezi kuandaa mechi hiyo Uwanja wa Nyayo wikendi hii kwa sababu serikali imeuhifadhi kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika Jumapili na Jumatatu. Tarehe mpya ya dabi hiyo itatangazwa na FKF.