Bandari hawapo Bongo kutalii
ZIARA ya Bandari FC nchini Tanzania ni mahususi kuboresha viwango vya wachezaji wao kuelekea mikikimikiki ya Ligi Kuu Kenya inayotarajiwa kung’oa nanga Agosti 26 mwaka huu.
Chini ya kocha mkuu Twahir Muhiddin, timu hiyo imekuwa kambini Bongo kwa siku 10 sasa na imeshacheza gemu moja dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kufanikiwa kushinda bao 1-0 lililofungwa na Shassir Nahimana.
Timu hiyo inatarajiwa leo Jumamosi usiku kucheza dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex uliyopo Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
“Tunataka kucheza dhidi ya Azam na kisha tunatafuta mechi ya kirafiki dhidi ya Singida Fountain Gate miongoni mwa timu zingine kwa lengo la kuwapima wachezaji wetu,” alisema kocha Muhiddin.
Kocha huyo alifichua wamepanga pia kucheza dhidi ya AS Vita Kigali ya Rwanda ambao pia wameweka kambi jijini Dar es Salaam akisisitiza gemu kama hizo dhidi ya timu bora ni jukwaa zuri kwa Bandari FC kupima uwezo wao kabla ya msimu mpya kuanza.
Naye Makamu Mwenyeki wa Bodi ya Bandari FC, Twaha Mbarak, alisema wanajipima na timu za viwango vya juu barani Afrika kwani lengo lao ni kujiandaa kurudi katika mshikemshike wa michuano ya Afrika ngazi ya klabu.
Mbarak alidokeza timu ikisharudi nchini kutoka ziara yake ya Bongo itaelekea Kaunti ya Kericho kuweka kambi kwa nia ya kuboresha vipaji vya wachezaji wao kimwili na kihisia.