Aussems: Januari ilikua ngori

KOCHA wa AFC Leopards, Patrick Aussems, amesema kikosi chake cha wachezaji chipukizi kimecheza mechi nyingi mwezi uliopita na wiki hii watacheza mechi mbili ndani ya siku nne.

Ingwe ambao walitoka kuwalizimisha mashemeji zao Gor Mahia sare tasa mwishoni mwa wiki iliyopita, jana katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi walikua wanaikabili Vihiga Bullets na Jumapili watakua na mechi ugenini Uwanja wa Sudi kaunti ya Bungomo dhidi ya vinara wa FKFPL, Nzoia Sugar.

Aussems alisema wingi wa mechi imekuwa changamoto kubwa kwa kikosi chake changa chenye wachezaji chipukizi na pia hana kikosi kipana kutokana na klabu hiyo kutumikia adhabu ya kutofanya usajili.

“Kwetu sisi, hakuna kitu muhimu kama ustawi wa wachezaji. Mechi zimekuwa nyingi sana na hiyo imefanya nyota wetu wachanga wachoke. Tunataka kuwapumzisha baadhi kuhakikisha wanaendelea kuwa freshi,” alisema Aussems.

“Ukiangalia kikosi changu kwasasa, sina wachezaji wengi wazoefu. Wengi wao ni wachanga halafu kikosi pia sio kipana. Tuna wachezaji kama 13 ama 14 wenye uwezo wa kucheza mara kwa mara, hii ilifanya Januari kuwa ngumu sana kwetu.”

Aussems aliiambia MWANASPOTI kuwa vijana wake waliteseka sana mwezi uliopita wakilazimika kucheza mechi saba ngumu ndani ya siku 25.

Katika mechi hizo saba, Ingwe ilipoteza mchezo moja tu dhidi ya Bidco United (4-1) na kutoa sare moja dhidi ya Gor Mahia huku wakiifunga Nairobi City Stars (1-0), Wazito FC (2-1), Mathare United (2-1), Bandari (2-0) na Police FC (1-0).