Aussems atuliza Ingwe

Muktasari:

  • MASHABIKI wa AFC Leopards sasa wanaweza kutuliza presha baada ya kocha mkuu wao, Patrick Aussems ‘Uchebe’, kuwahakikishia atarudi tena kuiongoza Ingwe kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Kenya msimu huu.

MASHABIKI wa AFC Leopards sasa wanaweza kutuliza presha baada ya kocha mkuu wao, Patrick Aussems ‘Uchebe’, kuwahakikishia atarudi tena kuiongoza Ingwe kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Kenya msimu huu.

Aussems, raia wa Ubelgiji, alizua taharuki wiki iliyopita baada ya kuandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter anarudi kwao kwa siku chache kuijulia hali familia yake.

Kwa sasa Ligi Kuu Kenya imesimama kwa muda usiojulikana kutokana na agizo la Rais Uhuru Kenyatta ya kutaka shughuli zote za michezo nchini kusitishwa kama njia mojawapo ya kupambana na tandavu ya tatu ya msambao wa virusi vya corona.

Hata hivyo, wakati wa kuipokea kikosi cha timu ya taifa, Harambee Stars, kilichowasili nchini kutoka Togo waliposhinda mchezo wao wa mwisho kufuzu Kombe la Afrika mwakani 2-1, Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nick Mwendwa, alidokeza wapo kwenye mazungumzo na wasimamizi wa Wizara ya Michezo kuona ni namna gani ligi itarudi tena.

Kocha wa Harambee Stars, Jacob ‘Ghost’ Mulee, anamatumaini ligi itarudi mapema ili kumpa fursa kuwatazama wachezaji wanaosakata soka la ndani kuelekea michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2022 itakayoanza Juni mwaka huu.

Aussems alitumia mwanya wa ligi kusimama kutimkia kwao akizua hofu miongoni mwa mashabiki wa Ingwe wengi wakiwa na kumbukumbu ya makocha hususan wa kigeni kutumia kigezo cha kwenda kusalimia familia na kisha kutokomea huko wasirudi tena.

“Kutokana na kusitishwa kwa michezo, narudi nyumbani kwa siku chache kusalimia familia. Nitarudi pindi ligi itakapoanza tena. Nina matumaini itakua hivi karibuni,” aliandika Uchebe kwenye ukurasa wake wa twitter.

Ni andiko lililomuibua Seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja, akimsihi Mbelgiji huyo kutokuiacha AFC Leopards.

Sakaja ambaye ni moja wa mashabiki sugu wa Ingwe alimtaka Aussems ahakikishe anatimiza ahadi yake ya kurudi pindi shughuli za michezo na hususan ligi itakaporejea tena.

Aussems alituliza presha ya Sakaja na mashabiki wa Ingwe alipoandika kwa mtandao wake wa twitter hamu yake ya kurudi Nairobi na kumalizia kazi kubwa ikiwa ni kuleta kombe ndani ya himaya ya AFC Leopards.

Aidha Uchebe ambaye alipata mafanikio akiifundisha Simba ya Tanzania aliyoiongoza kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/19, alithibitisha kupata chanjo ya kukabiliana na makali ya virusi vya corona.

“Tayari nimeshapata chanjo ya kwanza! Namshukuru daktari wangu na jiji langu la Bellegrade, Gard nchini Ufaransa! Nina hamu ya kurudi Nairobi na kumalizia kazi ili kuwapa AFC Leopards kombe nikishapata tu chanjo ya pili siku chache zijazo,” aliandika Uchebe.