Aussems atoa kali ya mwaka

KOCHA wa AFC Leopards, Patrick Aussems, alisema staili ya uchezaji ya Bidco United ndiyo iliyochangia timu yake kupokea kichapo cha mabao 4-1 mwishoni mwa wiki iliyopita.
Aussems ambaye alishuhudia Ingwe ikipoteza mchezo wa tatu msimu huu alidai mtindo wa uchezaji wa Bidco haupo kabisa kwenye ulimwengu wa soka.
Mabao ya Bidco katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi yalifungwa na Eric Gichumu, Francis Odour na Henry Juma aliyetupia mawili akitokea benchi huku lile la kufutia machozi la Ingwe likifungwa na Ola Olaniyi.
Aussems alikashifu staili ya mchezo wa Bidco kwa kudai kila timu wanayokutana nayo hucheza kwa mbinu hiyo dhidi yao.
“Timu zote hizi tulizochuana nazo, wakikutana na sisi mbinu yao huwa ni mipira mirefu na kucheza rafu. Ndio sababu tunalemewa. Hiyo sio soka kabisa, mpira hauchezwi hivyo, staili gani hiyo ya kihuni. Itabidi sasa tutafute mbinu ya kukabiliana na staili hii,” alilalama kocha huyo raia wa Ubelgiji.
Hata hivyo Aussems pia alitupia lawama mabeki wake kwa kushindwa kuwasiliana na kuruhusu mabao mepesi.
Kipigo hicho kimewaacha Ingwe katika nafasi ya 10 kwa pointi nane baada ya mechi saba huku Bidco wakikamata nafasi ya 12 kwa alama saba kutokana na idadi sawa ya mechi.