6 ndani ya pre-season tamu

HUKU msimu mpya wa Ligi Kuu Kenya ukisubiriwa kwa hamu, klabu sita za FKFPL zimeandaa dimba la pre-season itakayotoa zawadi ya Sh1 milioni kwa mshindi.
Dimba hilo lililopewa jina la Elite Pre-season Cup Tournament, linaanza leo na litafikia tamati Jumapili kwa kushirikisha Kariobangi Sharks, Ulinzi Stars, Sofapaka, Kenya Police, Gor Mahia na Nairobi City Stars.
Ngoma hiyo itakayopigwa katika Uwanja wa Utalii uliyopo Kasarani jijini Nairobi imeshuhudia timu hizo sita zikipangwa kwa makundi mawili.
Ulinzi Stars chini ya kocha mpya Bernard Mwalala wapo Kundi A inayojumuisha, Sharks na Sofapaka wakati Kundi B inatimu za Kenya Police, Gor Mahia na City Stars ambapo mechi ya ufunguzi inawakutanisha wanajeshi wa Ulinzi Stars dhidi ya Sharks kabla ya Police FC kuwakabili K’Ogalo.
Kesho ni zamu ya Gor kuchuana na City Stars kisha Sharks wapepetane na Sofapaka kabla ya mechi za makundi kuhitimishwa Alhamisi na kutakuwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tano na sita Ijumaa, nusu fainali ikipigwa Jumamosi na jamvi la pre-season hiyo tamu kuhitimishwa Jumapili mshindi akiponyoka na doo safi hiyo.