Zoran aipiga mkwara Yanga

SAA chache kabla ya kutesti mitambo dhidi ya St George ya Ethiopia katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya kuhitimisha Tamasha la Simba Dar, Kocha Zoran Maki amezichimba mkwara timu pinzani ikiwamo Yanga kwamba, ana kikosi bora na kitakachowasumbua katika Ligi Kuu Bara.

Simba itaanza msimu mpya ikiwa na Zoran wikiendi ijayo kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, huku ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 ilichopewa na watani wao hao kwenye mchezo kama huo uliofanyika mwaka jana, bao likiwekwa kimiani ya Fiston Mayele.

Licha ya kujua ugumu wa pambano hilo, Kocha Zoran alisema mechi nne za kirafiki ilizocheza timu hiyo ikiwa Misri na ya ule wa leo dhidi ya St George zitamsaidia kupata mwanga hasa kulingana na aina ya wachezaji iliyonayo kikosini kwa sasa.

Ikiwa kambini Mwanaspoti lilibaini kwamba kocha huyo alikuwa akitumia mifumo mitatu tofauti, huku miwili akiitrumia zaidi ambayo ni ile ya 4-3-3 na 4-2-3-1 iliyotumika tangu msimu uliopita, lakini ikionekana wazi huenda kukawa na mabadiliko machache kwenye upangwaji wa timu.

Kipa Aishi Manula pamoja na mabeki wa pembeni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ huenda wakasalia kikosi cha kwanza, huku eneo la beki wa kati mmoja kati ya Henock Inonga na Joash Onyango atalazimika kukaa benchi ili kumpisha Mohamed Ouattara aliyeonyesha uwezo mkubwa tangu atue kambini Misri.

Katika kiungo Jonas Mkude amerejea kwenye ubora wake na kuwapa kazi Victor Akpan, Erasto Nyoni, Nassor Kapama na Mzamiru Yasin ambaye hakuwepo kambini kuchuana kupata nafasi kikosini, lakini eneo la mbele Moses Phiri, Augustine Okrah, Clatous Chama, Pape Sakho na Pater Banda kila mmoja ana nafasi ya kupenya mbele ya Zoarn, japo Okrah, Chama na Sakho wanaonekana kuwa katika kikosi cha kwanza. Chaguo la pili linaweza kuangukia kwa Phiri na Banda, wakati kwenye ushambuliaji Nelson Okwa aliyetambulishwa hivi karibuni, Habib Kyombo, Denis Kibu na John Bocco mbali na straika Dejan Georgijevic aliye mbioni kutambulishwa rasmi.

Kocha Zoran amemsifia Okwa na kusema nji mchezaji mwenye kiwango anayeamini ataibeba timu huku, pia akisema kwa ujumla Simba aliyonayo ni timu bora na haina hofu ya kukutana na timu yoyote kwani wana malengo ya kufunika michuano ya ndani na ile ya kimataifa.


MSIKIE ZORAN

Zoran alisema anapenda kutumia mfumo wa 4-3-3, kutokana ni mzuri kwenye kushambulia pamoja na kuzuia mashambulizi ya timu pinzani na kusema soka lake ni kushambulia mwanzo mwisho hali ambayo itaifanya timu hiyo kukabiliana na timu yoyote ikiwamo Yanga itakayocheza nao Agosti 13.

“Tutakwenda kucheza kwa mfumo huo na wachezaji wengi niliokuwa nao wanafiti katika kile tunachohitaji ingawa katika baadhi ya mechi tutakuwa tukibadilika uchezaji wetu pamoja na wachezaji kwani wengi ni bora na wanastahili kucheza kikosi cha kwanza,” alisema na Zoran na kuongeza;

“Katika mechi za ugeni nafahamu viwanja vingi eneo la kuchezea huko siyo zuri kwa maana hiyo tutabadilsha uchezaji wetu na wachezaji ila mpira wetu wa kushambulia kwa haraka hautaondoka na tunafanya yote hayo ili kuhakikisha tunashinda na kufanya vizuri.”

“Simba kuna wachezaji wengi wenye ubora katika maeneo mengi ni wazi kuna mabadiliko yatakuwa yakifanyika kwa wachezaji ili kutoa nafasi kila mmoja kuonyesha ubora wake na mchango wa kusaidia timu, ngoja tuone michuano ikianza, ila Simba inataka kurejesha heshima.”