ZILITRENDI: Yanga yamponza Kado
KATIKA tarehe kama ya leo ya Machi 24, mwaka 2008 iliripotiwa stori juu ya kipa Shaaban Kado aliyekuwa akiidakia Moro United kuingia matatani na kusimamishwa na timu yake kutokana na mabao mawili aliyofungwa na Yanga katika Ligi Kuu Bara.
Kado alikumbana na kisanga hicho sikuchache baada ya Yanga kuifumua Moro United kwa mabao 2-1 mjini Morogoro na kumpa kesi kipa huyo mbele ya mabosi wake akionekana kama aliyeihujumu na kusimamishwa pamoja na beki John Njama.
Wachezaji hao walikuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Ally Jangalu, walisimamishwa kwa madai ya utomvu wa nidhamu pamoja na kuihujumu timu hiyo ikafungwa na Yanga.
Habari zilizopatikana mjini Morogoro wakati huo na kuthibitishwa na meneja wa timu hiyo, Willy Manekana zilisema wachezaji hao walikabidhiwa barua zao za kusimamishwa tangu Machi 15 na nakala kuwasilishwa kwa Chama cha Soka mkoa wa Morogoro (MRFA).
"Wachezaji hao wamesimamishwa na kupewa barua zao tangu wiki iliyopita na hawapo kambini kutokana na utomvu wa nishamu na michezo yetu iliyosalia tutamtumia kipa Noel Pompi," alisema Manekana ambaye alikataa kuzungumzia zaidi sakata hilo.
Kado kwa sasa ni kipa wa Mtibwa Sugar, lakini akiwahi kukipiga pia Yanga na Coastal Union na Mwadui.