ZILITRENDI: Sangoma wa Simba alia kutapeliwa

EBWANAEEE, kama kawaida tunaendelea na mastori yaliyowahi kutrendi nchini miaka kibao iliyopita na safari hii tunalisongesha hadi 2001 lakini katika tarehe kama ya leo ya Februari 24.
Unaambiwa siku hiyo kuna stori ilibamba kinoma ilityohusu mpiga tunguri anayedaiwa kutumiwa na Simba kufanikisha ushindi wa mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Tusker dhidi ya Yanga.
Mwanaspoti lilipoti stori hiyo ikisema wiki chache baada ya ushindi wa penalti 5-4 iliyopata Simba dhidi ya Yanga katika fainali hiyo ya Tusker 2001, , Mganga wa kienyeji aliyetumiwa na Simba 'kuroga' mchezo huo amelalamika kwamba uongozi wa timu hiyo umemdhulumu Sh1milioni.
KOLAMU YA ENZI HIZO IMEHAMA KUTOKA GAZETI LA JUMAPILI HADI KILA ALHAMISI
Akizungumza na Mwanaspoti nyumbani kwake Vingunguti Dar es Salaam, Sangoma huyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema kabla ya mchezo huo wa fainali ya Kombe la Tusker viongozi wa Simba walimfuata ili 'aroge'.
Mganga huyo alisema Simba walimuahidi kiasi hicho cha fedha, lakini mara baada ya ushindi kwenye mchezo huo na kushinda kitita cha Sh 15Milioni iliyokuwa zawadi wa bingwa wa michuano, hakuwaona tena kumalizia deni lao.
"Lakini cha ajabu ni kuwa ilipofika Februari 16, viongozi wa Simba walikuja tena na kuniambia niwasaidie ili washinde mchezo wao na Yanga (kugombania Ngao ya Hisani), ila nikawakatalia."
Sangoma huyo alisema aliwataka viongozi wa Simba kuingia mkataba mpya ikiwa pamoja na kulipa kwanza Sh 1milioni za awali kabla ya kuwafanyia kazi wanayoitaka, lakini wakaingia mitini
Katika mchezo huo wa kuwania Ngao ya Hisani iliyotolewa na kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) Yanga ilishinda mabao 2-1 na kufanikiwa kutwaa taji hilo na kitita cha Sh 10milioni.
"Inaelekea wana matatizo makubwa katika uongozi wao na ndio maana hawajanilipa fedha zangu, lakini mimi sitowafanyia kitu chochote zaidi ya kumwachia Mungu," alisema.
Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Dewji alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo alidai kuwa hajui chochote na wala hamfahamu mganga huyo na kwamba hawana fungu la kuwalipa waganga.
"Unajua mashabiki wanapenda mambo hayo, inawezekana kuna baadhi yao walifanya hivyo lakini sio klabu, labda mwenyekiti, Juma Salum anaweza kujua zaidi kuhusu hilo."
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu jana kutoka Mbeya, Juma Salum alisema hajui chochote kuhusu hilo na kudai walipata ushindi wao kihalali na wala sio kwa kutumia Sangoma.
"Tungekuwa tunaamini mambo hayo tusingeagiza kocha kutoka Kenya (James Siang'a) na kama huyo mganga anatudai basi anaweza kwenda mahakamani kutushitaki."
Alidai kwamba toka wametwaa Kombe la Tusker wamekuwa wakiletewa madeni mbalimbali ambayo hawayajui.