ZILIPENDWA ; Mafisango: Simba nilipeni changu nirudi kwetu
Muktasari:
Mafisango alikuwa Mnyarwanda mwenye asili ya DR Congo, alisimamishwa kwa kile kinachodaiwa ni utovu wa nidhamu. Inadaiwa aliripoti kambini maeneo ya Bamba Beach, Kigamboni jijini Dar es Salaam akiwa amelewa chakari, akanaswa na meneja wake Nico Nyagawa.
BAADA ya kusimamishwa na uongozi wa Simba, Patrick Mafisango, sasa anataka alipwe ili arudi kwao Rwanda.
Mafisango alikuwa Mnyarwanda mwenye asili ya DR Congo, alisimamishwa kwa kile kinachodaiwa ni utovu wa nidhamu. Inadaiwa aliripoti kambini maeneo ya Bamba Beach, Kigamboni jijini Dar es Salaam akiwa amelewa chakari, akanaswa na meneja wake Nico Nyagawa.
Inaelezwa badala ya kujieleza aliwarushia maneno yasiyo ya kiungwana Nyagawa na Kocha Milovan Cirkovic na inadaiwa Mserbia huyo ndiye aliuarifu uongozi ukaamua kumwondoa kambini.
Lakini, Mafisango alipozungumza na mwandishi Doris Maliyaga nyumbani kwake Keko, Dar es Salaam na habari hii ikachapishwa tarehe kama ya leo Aprili 2, 2012, alisema: “Nimechoka na majungu, kuna watu wanataka kuniharibia jina. Ninachotaka sasa, Simba inilipe haki zangu zilizobaki kabla ya mkataba wangu kuisha. Nauli ya mtoto wangu (Crespo), mke wangu na mimi, nirudi nyumbani nikafanye mambo mengine.”
“Majungu haya yapo Tanzania tu, mbona nimecheza Rwanda na DR Congo hakukuwa na matatizo kama haya,” alisema Mafisango.
Hata hivyo, hazikupita siku nyingi, Mafisango alipata ajari ya gari na kufariki hapo hapo na ilikuwa usiku wa Mei 17, kuamkia 18. Mafisango alipata ajali hiyo maeneo ya Keko, Dar es Salaam na kuzikwa kwao, DR Congo.