Zilikuwa siku 10 za kibabe Mapinduzi Cup 2024

LADY Jaydee aliwahi kuimba wimbo usemao ‘Siku Hazigandi’. Huwezi kumbishia, ni kweli siku huwa hazigandi, kwani hata huko kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 siku zinazidi kuyoyoma. Ndio, ilianza Desemba 28 ikishirikisha jumla ya klabu 12, lakini leo Jumamosi ikiwa ni mapumziko hesabu zikionyesha siku 10 zimeshaenda na maji na zimeondoka na timu mbili zilizokuwapo awali.
Kwa sasa michuano imesaliwa na wiki moja tu kabla ya bingwa wa michuano hiyo atakapofahamika rasmi pale itakapopigwa mechi ya fainali, Januari 13.
Vital’O ya Burundi iliyoshiriki kwa mara ya kwanza na JKU ndizo zilizoaga mapema, wakati Chipukizi, Jamhuri na Jamus iliyokuwa uwanjani jana jioni zilikuwa zikiomba itokee miujiza ili zisiwe miongoni mwa timu mbili za mwisho kuaga michuano hiyo ili kupisha robo fainali.
Jamus iliyopo Kundi C ilikuwa na pointi moja wakati Jamhuri iliyokuwa ikicheza nayo jana jioni haikuwa na pointi, hivyo kama Jamhuri ingeshinda ingekuwa na uwezo wa kufikisha pointi tatu na kuwang’oa Wasudan Kusini na kwenda robo fainali.
Kama Jamusi imeshinda itafikisha pointi nne na kwenda kama best looser na kuitupa nje Jamhuri na kama timu hizo zimetoka sare zingeungana na Chipukizi iliyomaliza nafasi ya tatu katika Kundi A kwani kila moja ingemaliza na pointi mbili na kuangaliwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ili kuungana na timu saba kutinga robo fainali zitakazochezwa rasmi kesho Jumapili na Jumatatu.
Hapa chini ni uchambuzi wa siku tisa za mechi za makundi na namna mambo yalivyokuwa wakati mashabiki wakijiandaa kushuhudia uhondo wa michezo ya robo fainali inayopigwa kesho na Jumatatu.
WANAUME WA SHOKA
Klabu nane zilizopenya kwenye robo fainali ni Azam FC iliyoongoza msimamo wa Kundi A ikikusanya pointi saba na mabao manne na kufungwa moja, huku ikifuatiwa na Mlandege ambao ni watetezi wa taji waliovuna alama tatu tu kupitia sare tatu ilizopata kwenye mechi ilizocheza.
Azam ilipata ushindi kwenye mechi mbili dhidi ya Chipukizi na Vital’O na kulazimishwa sare na Mlandege, iliyotoka sare pia na wapinzani wengine wa kundi hilo ambalo kila mmoja ilimaliza na pointi mbili na kuing’ioa Vital’O kupenya kwenye mshindwa bora (best Looser).
Kutoka Kundi B, Simba iliyokuwa uwanjani usiku wa jana kumalizana na APR ya Rwanda tayari imeshafuzu kama ilivyo kwa Singida Fountain Gate iliyomaliza mechi za kundi hilo ikiwa na pointi sita, ikishinda michezo miwili dhidi ya JKU na APR na kunyukwa na Simba.
Simba ilishajikusanyia pointi sita (kabla ya mechi ya jana usiku) na kujihakikisha nafasi ya kwanza baada ya kuzitungua JKU na Singida, wakati APR waliokuwa wakivaana nao jana usiku, ilikuwa na pointi tatu baada ya kuifunga JKU, iliyoaga kwa aibu michuano hiyo bila kupata pointi moja.
Matokeo yoyote yaliyopatikana jana yalikuwa yakibadilisha tu labda msimamo, lakini timu hizo tatu za Simba, Singida na APR ambayo inaweza kuingia kama best looser, zilikuwa zimeshafuzu.
Kundi C lenyewe pia limepenyeza timu mbili za Yanga, KVZ, huku Jamus ya Sudan Kusini ambayo iliingizwa kwenye michuano hiyo dakika za mwisho kama ilivyo kwa JKU, ilikuwa ikimalizana na Jamhuri ili kuwania nafasi moja ya best looser kutoka kundi hilo na bila shaka matokeo tayari unayo.
MABAO KIBAO
Kabla ya mechi za jana, michuano hiyo ilishuhudia jumla ya mabao 40, likiwamo moja la kujifunga na yalikuwa yamefungwa katika mechi 16 za makundi kupitia wachezaji 30, huku Alassane Diao wa Azam FC na Elvis Rupia wa Singida wakiwa ndio vinara kila mmoja akifunga mabao matatu.
Wachezaji sita tofauti wameshika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mawili kila mmoja, huku wachezaji wengine 21 wakitupia bao moja kila mmoja na beki wa JKU, Mohamed Hassan akiwa pekee aliyetupia mpira nyavuni mwa lango la timu yake wakati wakishindiliwa mabao 3-1 na Simba.
Katika mabao 39 yaliyofungwa na wachezaji wengine kwenye milango ya wapinzani, sita ni ya penalti, huku Saleh Abdallah wa JKU akiongoza kwa kufunga mikwaju miwili na kuifanya timu hiyo kuwa vinara wa kupata penalti nyingine katika msimu huu wa 18 wa michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007.
Timu nyingine zilizopata penalti ni Jamus, Singida, Chipukizi na Vital’O zilizopata moja moja, huku timu za APR, Simba, Yanga, KVZ, Jamhuri, Azam na Mlandege zikiwa ndizo hazikubahatika kupewa penalti katika mechi hizo za makundi.
Katika mechi hizo Yanga na Singida ndizo timu zilizotoa vipigo vikubwa (kabla ya mechi za jana) huku mechi tatu pekee zilizoisha bila kufungwa bao lolote ikiwemo ile ya juzi kati ya Yanga na KVZ, Azam na Mlandege na Vital’O na Chipukizi.
Yanga ilianza kwa kishindo ikishinda mabao 5-0 dhidi ya Jamhuri, huku Singida ikiinyoa JKU mabao 4-1 zikiwa ndizo mechi zilizokuwa na mabao mengi zikifuatiwa na zile za Singida na APR (3-1), Azam na Vital’O (3-1) na ile ya Simba na JKU (3-1).
DIAO NA KIPA
Katika mechi hizo 16, Alassane Diao wa Azam na kipa wa Chipukizi, Suleiman Abrahman wamefunika kwa kutangazwa ‘Nyota wa Mchezo’ mara nyingi zaidi ya wachezaji wengine, wakifanya hivyo mara mbili kila mmoja kati ya mechi tatu za timu zao.
Diao aliyefunga mabao matatu, alichaguliwa katika mechi dhidi ya Chipukizi na Vital’O wakati Kipa huyo aling’ara kwenye mechi dhidi ya Vital’O na Mlandege na kuwafunika wachezaji wengine 14 waliotangazwa mara moja moja kwenye mechi hizo 16 (kabla ya michezo miwili ya jana).
Wachezaji wengine waliong’ara ni; Yannick Bangala (Azam FC), Akram Omar ‘Haaland’ (KVZ), Elvis Rupia (Singida FG), Abdallah Kulandana (Mlandege), Omer Michael (Jamus), Crispin Ngushi (Yanga), Morice Chukwu (Singida FG), Fondoh Che Malone (Simba), Benjamin Laku (Jamus), Niyibizi Ramadhan (APR), Fabrice Ngoma (Simba) na Salum Athuman Salum wa KVZ (kabla ya mechi za jana).
REKODI YA AKRAM
Nyota wa KVZ, Akram Omar Muhina ‘Haaland’ ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la kwanza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, uliozinduliwa rasmi Desemba 27, mwaka jana kwa pambano la kirafiki la timu za taifa za Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes ya Zanzibar, mechi iliyoisha kwa suluhu.
Hata michuano ya Mapinduzi ilipoanza siku inayofuata yaani Desemba 28, Azam na Mlandege zilishindwa kufungana kama ilivyokuwa kwa Vital’O na Chipukizi.
Lakini siku ya pili ya michuano hiyo katika mechi ya tatu kati ya KVZ na Jamhuri, Haaland huyo wa Zanzibar alifunga bao la kwanza na kuongeza jingine la pili lililoiwezesha maafande wa KVZ kushinda 2-0 na mchezaji huyo kuondoka uwanjani akiwa ‘tajiri’ kwani alinyakua Sh1 milioni za kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye uwanja huo uliokarabatiwa na kuwa na mwonekano mpya wa kisasa.
Pia alivuna Sh500,000 za kuwa Nyota wa Mchezo huo kwa mabao hayo mawili aliyowatungua Jamhuri, hivyo kumfanya siku hiyo kuvuna Sh1.5 milioni.