ZFF yapangua 32 Bora Kombe la FA

Muktasari:
- Mabadiliko hayo yamekuja huku kukiwa na malalamiko mengi kwa baadhi ya wadau na mashabiki wa soka Zanzibar wakilalamikia mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) wakati mwingine bila ya kutolewa kwa taarifa mapema na kuwachanganya.
KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), imepangua ratiba ya mechi za michuano ya Kombe la FA hatua ya 32 Bora iliyokuwa ianze Jumatatu wiki ijayo, Machi 4 na sasa itaanza kupigwa kuanzia Machi 5-9.
Mchezo uliopanguliwa kwenye michuano hiyo inayotoa bingwa anayeiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ni ule unaozihusisha timu za Malindi dhidi ya Nangobo na JKU dhidi ya Union Rangers ambazo zote zilipangwa kupigwa Machi 4 kabla ya kusongezwa mbele kwa siku moja.
Katibu wa Kamati ya Mashindano ya ZFF, Ali Bakar 'Cheupe' amefafanua sababu ya mabadiliko hayo akisema yamekuja kufuatia Bodi ya Ligi Zanzibar kufanya mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu, ili kuwani mfungo wa Mwezi wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza kati ya Machi 11-12 kulingana na mwandamo wa mwezi.
"Bodi ya Ligi imefanya mabadiliko ya ratiba siku hiyo ambayo tulikuwa tuanze michezo hiyo ya 32 Bora ya FA, hivyo tumeona ni bora ianze Machi 5 na ile michezo iliyokuwa ichezwe siku ya kwanza yaani Machi 4 kupelekwa Machi 9," amesema Cheupe.
Mabadiliko hayo yamekuja huku kukiwa na malalamiko mengi kwa baadhi ya wadau na mashabiki wa soka Zanzibar wakilalamikia mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) wakati mwingine bila ya kutolewa kwa taarifa mapema na kuwachanganya.
Ndani ya duru la pili takriban michezo minne ya Ligi Kuu imebadilishwa tarehe tofauti na ratiba inavyosomeka jambo ambalo liifanya kuwa ni changamoto kwa mashabiki wanaofuatilia ligi hiyo.
Baadhi ya michezo hiyo ni ule mchezo wa Mafunzo dhidi ya Jamhuri FC uliokuwa uchezwe Febuari 6 ukapigwa Febuari 9, huku Hard Rock na Kipanga zilizokuwa zikipigwe leo zikicheza jana bila mashabiki kuelezwa mapema.
Mohammed Khamis, mdau wa soka amesema mabadiliko ya ratiba yanaweza kuwa ni sababu ya Ligi Kuu kukosa mashabiki, kwani mechi zimekuwa zikibadilishwa hovyo kuliko hata michuano ya mchangani.
"Sikumbuki ulikuwa mchezo wa timu gani lakini ni Ligi Kuu tulifika uwanjani na baadhi ya mashabiki kuja kuangalia hiyo mechi. Kufika getini tukaambiwa huo mchezo ulichezwa jana," amesema shabiki huyo aliyeongeza kuwa ni vyema Bodi ya Ligi ikafuata ratiba ambayo waliipanga na kama kutakuwa na mabadiliko watoe taarifa mapema ili kuepusha usumbufu.
Bodi ya Ligi kupitia Mtendaji Mkuu, Issa Kassim amesema mabadiliko mara nyingi hutokana na timu kuomba mechi zirudishwe nyuma hususan zikiwa ugenini kutokana na kukosa fedha za kujikimu.
"Timu ambazo zitatoka Pemba kuja hapa Unguja na zile za hapa Unguja zikienda Pemba huwa zinakubaliana michezo ichezwe papo kwa papo kwa sababu viongozi wanakuwa hawana fedha za kutosha. Kwa hiyo hawawezi kukaa muda mrefu ugenini," amesema.