Zamalek yakacha Azam complex, yalipa Sh 116m

Zamalek yakacha Azam complex, yalipa Sh 116m

MABINGWA mara 20 wa Ligi Kuu nchini Misri, Zamalek wameilipa Dola za Kimarekani 50,000 (Sh 116milioni) kwa klabu ya Burundi ya Flambeau du Centre kwa kukubali kucheza mechi zote mbili za hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika nchini Misri kwenye Uwanja wa Borg El Arab.

Hapo awali klabu hiyo ilitarajiwa kutua jijini Dar es Salaam wiki hii kwaajili ya mchezo wao dhidi ya Flambeau katika mchezo wao uliopangwa kuchezwa kwenye uwanja wa Azam Complex huku wenyeji wa mchezo huo nao walitarijiwa kutua nchini hii leo kwa mujibu taarifa za hapo awali.

Hata hivyo mabingwa hao wa Burundi usingekuwa mchezo wao wa kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex kwani mechi yao dhidi ya Al Attihad ya Libya walicheza kwenye uwanja huo ambapo waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Taarifa kutoka ndani ya Zamalek zinasema kuwa wangetumia zaidi ya Dola 203,468 kama wangetua hapa nchini kwaajili ya mchezo huo wa mkondo wa kwanza.
Naye Rais wao  Mortada Mansour amewapa wachezaji wa kikosi cha kwanza zaidi ya Dola 1milioni huku akitoa dola 407,000 kwa Wafanyakazi, benchi la ufundi na wasimamizi wa klabu hiyo ili wagawiwe kabla ya mchezo huo.