Zahera ampa Mzize mchongo wa ughaibuni

Muktasari:

  • Zahera amefunguka hayo siku chache baada ya Azam FC kupeleka ofa ya Sh400 milioni Yanga ili kuipata saini ya mshambuliaji huyo anayeinukia ili atue Chamazi msimu ujao.

KOCHA wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera amemshauri mshambuliaji, Clement Mzize kuondoka Tanzania ili kwenda kuongeza ujuzi nje ya mipaka.

Zahera amefunguka hayo siku chache baada ya Azam FC kupeleka ofa ya Sh400 milioni Yanga ili kuipata saini ya mshambuliaji huyo anayeinukia ili atue Chamazi msimu ujao.

"Mimi ndiye niliyempandisha Mzize aweze kuchezeshwa katika timu ya wakubwa baada ya kuona kipaji chake, namshukuru aliyekuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi kwa kumkubali na kumpa nafasi ya kucheza kama 'sub' wa Fiston Mayele," alisema na kuongeza;

"Hakuna mabadiliko ya kiuchezaji yatatokea kwake kama ataendelea kubali Tanzania, timu yoyote inayoshiriki ligi ikifikia muafaka wa kumchukua nasisitiza ataendelea kubaki katika nafasi aliyopo sasa, hawezi kukua," alisema Zahera.

Zahera alisema ili aweze kubadilika kutokana na umri wake anatakiwa kuondoka Tanzania kwenda kujaribu maisha mengine na changamoto mpya za kiuchezaji.

"Kule kwanza atapata faida kuanzia namna ya mazoezi uwanjani kwani kuna utofauti mkubwa zaidi na timu zetu hapa Tanzania, uwezo wa watu ambao watampokea na namna ya ufundishaji wao atakuwa na uwezo mzuri zaidi," alisema na kuongeza;

"Kama ni kweli ana ofa za kwenda nje na ana uhakika anaenda kucheza sio kufanya majaribio, namuona mbali sana kwani ana mwili mzuri wa kucheza, ana akili ya mpira na ana nguvu za kukabiliana na mabeki," alisema.

YANGA WAMPE KIPAUMBELE
Zahera pia amewaomba Yanga kuendelea kumuamini mshambuliaji huyo na kumpa kipaumbele kama mchezaji muhimu.

"Kama ilivyokuwa kwa Mayele alikuwa amekabidhiwa eneo la ushambuliaji, walikuwa wanamtegemea yeye, hivyo ndivyo inavyotakiwa kufanyika pia kwa Mzize ili ajitengenezee umuhimu kikosini, itamsaidia kuwa bora zaidi," alisema na kuongeza;

"Mchezaji kama anafahamu kuwa anategemewa kikosini anakuwa na aina tofauti ya kujiandaa tofauti na yule asiye na uhakika kama ilivyo kwa Yanga sasa, leo unamuona Keneddy Musonda kesho Mzize," alisema.

Zahera ambaye ni kocha wa Namungo, alisema Mzize ni mchezaji mzuri na kabla ya haya yote yanayoendelea yeye alishamtabiria kuwa atakuja kuwa mchezaji mkubwa ndani ya miaka miwili au mitatu mbele na sasa ndicho anachokiona kwake.